RC aipa siku 30 halmashauri kukamilisha madawati

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga

Muktasari:

  • Brigedia Jenerali mstaafu Maganga amesema hayo baada ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hanji Godigodi kukiambia kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Kigoma (RCC), kuwa hadi sasa kuna upungufu wa madawati 1,783 katika shule mbalimbali.
  • “Hakikisheni kazi hiyo ya madawati inakamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu, vinginevyo sitawavumilia kwa sababu kazi hii ilipaswa kuwa imekamilika mwaka jana,” amesema Maganga.

Kigoma. Mkuu wa Mkoa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga ameagiza kuwa ifikapo mwezi Mei, mwaka huu kazi ya kutengeneza madawati kwa Halmashauri ya Kigoma inapaswa kuwa imekamilika.

Brigedia Jenerali mstaafu Maganga amesema hayo baada ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hanji Godigodi kukiambia kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Kigoma (RCC), kuwa hadi sasa kuna upungufu wa madawati 1,783 katika shule mbalimbali.

“Hakikisheni kazi hiyo ya madawati inakamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu, vinginevyo sitawavumilia kwa sababu kazi hii ilipaswa kuwa imekamilika mwaka jana,” amesema Maganga.

Awali, Mbunge wa Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsanzugwanko alisema katika halmashauri ya mji Kasulu kuna ziada ya madawati, hivyo Kigoma inaweza kuomba kwa kufuata taratibu za kiofisi ili wapewe au kuazimwa.

Amesema alilazimika kutumia fedha ya mfuko wa jimbo kugharamia utengenezaji wa madawati kwa kuwa lilikuwa ni agizo la Serikali, na kazi ilikamilika kwa asilimia 100.