RC amwagiza mkandarasi kuongeza nguvu ujenzi wa chujio la maji

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa

Muktasari:

Akizungumza alipofanya ziara ya ghafla kwenye mradi huo, Dk Mlingwa alisema mkandarasi huyo hajakamilisha ujenzi wa chujio hilo lililogharimu Sh1.4 bilioni licha ya kuwa muda aliopewa ulikwishamalizika mwaka 2015.

Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa amemtaka mkandarasi wa mradi wa chujio la maji Mugumu, Kampuni ya Pet Cooperation Limited kuwatumia wataalamu wa Manispaa ya Musoma kwa kuwa hana wataalamu wa kutosha.

Akizungumza alipofanya ziara ya ghafla kwenye mradi huo, Dk Mlingwa alisema mkandarasi huyo hajakamilisha ujenzi wa chujio hilo lililogharimu Sh1.4 bilioni licha ya kuwa muda aliopewa ulikwishamalizika mwaka 2015.

Meneja Ufundi wa Muwasa, Barton Kajigiri alisema mkandarasi aliomba kupewa muda Hadi Juni, hata hivyo kalenda yake ilionyesha kuwa kazi hiyo ingekamilika Mei mwishoni mwaka huu.

“Tarehe 10, 2, 2017 katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambacho kilishirikisha wataalamu kutoka ofisi ya mkandarasi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Muwasa, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mugumu (Muguwasa) na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri, mkandarasi aliahidi Juni angemaliza kazi, hata hivyo hakuna dalili,” alisema.