RC apiga marufuku kubomolewa nyumba Manyara

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mara amezuia ubomoaji wa  nyumba  300 ambazo ziliidhinishwa kubomolewa na madiwani wa mkoa  huo

 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amepiga marufuku uamuzi wa kubomolewa nyumba 300 za mtaa wa Maisaka mjini Babati, uliotolewa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji huo.

Pia, Mnyeti ametishia kulifungia shughuli zake baraza la madiwani wa halmashauri ya mji huo kutokana na kutoa uamuzi ambao hauna  maslahi kwa jamii.

Akizungumza leo na Novemba 19 na wananchi wa mtaa wa Maisaka, amesema  hakubaliani na sababu za kuvunja nyumba hizo za wananchi wa Maisaka zilizotolewa na mkurugenzi wa mji huo Fortunatus Fwema.

Amesema  maamuzi hayo mabovu yanasababisha wananchi waichukie serikali yao, ila yeye akiwa mkuu wa mkoa huo hatakubaliana na kitendo hicho.

"Siwezi kukubaliana na maamuzi ya kipuuzi yanayotolewa na madiwani kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na serikali yao," amesema  Mnyeti na kuongeza.

 

"Mnataka kubomoa nyumba za watu wanyonge kisha mnasimama majukwaani na kusema eti haya ni maelekezo ya Rais wenu ameagiza mbomolewe nyumba zenu na kusababisha wananchi waichukie serikali."

Amesema  anasitisha zoezi hilo kwani yeye hakubaliani na sababu zilizotolewa na Fwema na kusababisha nyumba hizo ziwekwe alama ya X na kutaka kubomolewa.

Amesema  sababu zilizotolewa za ujenzi holela kwenye eneo hilo hakubaliani nazo kutokana na watumishi wa halmashauri hiyo nao wamechangia kwani walipaswa kuchukua hatua tangu awali kwenye msingi kabla ya wananchi hao hawajajenga.

"Watu wanajenga nyumba wewe mkurugenzi na watumishi wa ardhi mlikuwa wapi, hii tabia ya kujifungia chumbani na kufanya maamuzi ya kuumiza watu, naipiga marufuku," amesema  Mnyeti.

Amesema  pia, atafuatilia baadhi ya maamuzi ya vikao vya baraza la madiwani ambayo yamekuwa yakiumiza wananchi wa Babati kwa kufanya mzaha na maisha ya watu.

Awali, Mkurugenzi wa mji huo Fortunatus Fwema alisema vikao vitatu halali viliridhia nyumba hizo kuwekewa alama ya X na kutaka kubomolewa.

 

Fwema alitoa sababu ya kubomolewa ni ujenzi holela kwani wananchi hao walijenga bila kupata vibali kutoka halmashauri ya mji huo.

Amesema  uamuzi huo ulipitishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani, kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

 

Mmoja kati ya wananchi wa mtaa wa Maisaka, Hassan Juma ambaye nyumba yake iliwekewa alama ya X alitoa shukrani kwa mkuu huyo wa mkoa aliyepiga marufuku nyumba zao kubomolewa.

Juma amesema  japokuwa madiwani wa halmashauri hiyo ndiyo viongozi wao waliowachagua kwa kuwapa kura, lakini wameshindwa kuwatetea hivyo kuwashangaza kwa kukubali nyumba zao kuvunjwa.

 

Mkazi mwingine Mary Ombay amesema yeye na familia yake walishikwa na sintofahamu ya mustakabali wa maisha yao baada ya nyumba yao kuwekewa alama ya X.

"Sisi tulijinyima kwa muda mrefu ili tuweze kujenga nyumba yetu lakini mwisho wa siku inawekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa, tunamshukuru mkuu wa mkoa kwa uamuzi wake wa kusitisha zoezi hilo," amesema Ombay.