RC apiga marufuku uuzwaji mashamba ya CDA

Muktasari:

  • Katika kusimamia agizo lake mkuu wa mkoa ameviagiza vyombo vya usalama kumkamata mtu yeyote atakayekiuka maagizo yake.

 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge amepiga marufuku uendelezaji wa viwanja, mashamba na mauziano mapya katika maeneo manne ambayo awali iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) iliyatenga kama mashamba.

Maeneo hayo ambayo yalitengwa na CDA kama mashamba ili kukidhi mahitaji ya kilimo na mifugo ni Ndachi, Mbwanga, Miyuji na Msalato

Akizungumza leo Februari 19 katika mkutano na wakazi wa eneo la Ndachi ambao wamekuwa na mgogoro wa ardhi miaka mingi, Dk Mahenge alisema amefikia uamuzi huo baada ya kupitia mapendekezo ya tume iliyoundwa kushughulikia mgogoro wa eneo la Ndachi.

‘’Nimetafakari na kujiridhisha sasa naielekeza Manispaa ya Dodoma kuzingatia dhana ya mamlaka ya upangaji katika kutekeleza majukumu ya iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA),”amesema.

Ameagiza manispaa kuandaa mpango wa uendelezaji wa eneo lote lililokuwa la mashamba kwa kuzingatia jitihada za Serikali zinazoendelea za kufanya mapitio ya mpango kabambe wa manispaa ili kukidhi matakwa ya uamuzi wa Serikali ikiwemo uhamishaji wa hatimiliki kutolewa kwa miaka 99.

Dk Mahenge ameagiza maandalizi ya mpango huo kuwashirikisha wenye mashamba, kiwanja kwenye zoezi zima la utambuzi wa maeneo hayo na kufanya mikutano itakayoshirikisha makundi yote ya wakazi katika eneo hilo ili kuwafahamisha makusudio na mpango kazi utakaotekelezwa.

“Manispaa ifanye kazi ya kuhakiki na kupata taarifa kamili za wananchi wote wenye viwanja vya makazi, misingi iliyojengwa, mapagale na nyumba katika eneo hilo kwa ajili ya kuweka kwenye ramani ya msingi.

Pia ametaka miliki zote zenye mikopo kutambulika na kuweka namna bora ya kuingizwa katika mpango na iweke mpango wa uendelezaji ikijumuisha wakazi wote wa eneo lililovamiwa  na lisilovamiwa.

Amesema  baada ya kukamilisha hayo yote manispaa itapeleka mapendekezo ya namna ya kugawa na kumilikisha maeneo kulingana na upimaji ambao umeainishwa.

Ameagiza maofisa ardhi wa wilaya zote za Dodoma kufika mjini hapa kwa ajili ya kuja kushirikiana na wale wa Manispaa ili kurahisisha zoezi hilo huku akitoa wiki tano kuanzia jana liwe limekamilika.

Pia ameagiza  kamanda wa Polisi mkoani Dodoma na vyombo vya ulinzi na usalama kumkamata mtu yeyote ambaye atajihusisha na maendelezo katika maeneo aliyoyataja.