RC ataka kiwanda kuongeza bei ya pamba

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema hayo alipoongoza kamati ya ulinzi na usalama kutembelea kiwanda hicho kuangalia hali halisi ya utendaji.

Tabora. Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora, ametakiwa kuongeza bei ya ununuzi wa pamba kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa kilo ili kuwavutia wakulima kupeleka bidhaa hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema hayo alipoongoza kamati ya ulinzi na usalama kutembelea kiwanda hicho kuangalia hali halisi ya utendaji.

Mwanri alikaririwa na Idara ya Habari (Maelezo) akisema upatikanaji wa pamba kwa wingi kwa ajili ya kiwanda hicho na uzalishaji wa nyuzi na kamba ambazo zina viwango bora, utawasaidia kuhimili ushindani katika masoko hivyo kutengeneza ajira kwa vijana na kuongeza mapato ya Serikali.

Alikitaka kiwanda hicho kuzalisha kwa wingi ili kuepuka majengo kugeuzwa maghala ya kuhifadhi bidhaa kama wanavyofanya baadhi ya waliobinafsishiwa viwanda nchini.

Pia, Mwanri alimtaka mmiliki wa kiwanda hicho kupeleka nakala ya mkataba wa ubinafsishaji ili kuona kama masharti yamezingatiwa.

Kiwanda hicho hivi sasa kina watumishi 24, badala ya 350 waliokuwepo awali.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Urveshi Rajani alisema yupo tayari kununua pamba yote ya wakulima mkoani hapa iwapo atahakikishiwa upatikanaji wa soko la bidhaa zake ikiwamo wakulima wa tumbaku kupitia Chama cha Ushiriki cha Wakulima wa Tumbaku (Wetcu).

Rajani alisema Wetcu wakinunua nyuzi zao wapo tayari kuhakikisha pamba yote inayolimwa Tabora wanainunua kwa bei nzuri na kuendelea kuboresha kulingana na wanavyouza.

Alitoa wito kwa Serikali kudhibiti uingizaji kinyemela bidhaa kutoka nje kama khanga ambazo zinazalishwa nje, lakini zinaandikwa kuwa zimetengezwa Tanzania hali inayochangia kudhofisha viwanda nchini.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dk Thea Ntara aliwataka watendaji kuhakikisha wanasimamia wakulima wazalishe pamba kwa ajili ya kukiwezesha kiwanda hicho kuwa na malighafi ya kutosha.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi alitoa wito kwa wazalishaji wa mazao mbalimbali ikiwamo tumbaku, korosho na kahawa kununua nyuzi za kiwanda hicho ili kuunga mkono juhudi za mwekezaji huyo na kumsaidia kungeza ajira.