RC awapigania wakulima wa tangawizi Same

Muktasari:

Akizungumza na wataalamu hao mwishoni mwa wiki iliyopita, Sadiki alisema usimamizi mzuri ni njia mojawapo ya kuifanya kampuni hiyo kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuingia katika ushindani wa masoko ndani na nje ya nchi.

Same. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki amewaagiza wataalamu wanaounda bodi ya Kampuni ya Wakulima wa Tangawizi Mamba wilayani hapa kuhakikisha wakulima wa zao hilo wananufaika nalo.

Akizungumza na wataalamu hao mwishoni mwa wiki iliyopita, Sadiki alisema usimamizi mzuri ni njia mojawapo ya kuifanya kampuni hiyo kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuingia katika ushindani wa masoko ndani na nje ya nchi.

“Tunataka mzalishe bidhaa nzuri itakayowavutia wateja, kauli ya Tanzania ya viwanda inatokana na viwanda hivi vidogo msifikiri ni uanzishwaji wa viwanda vikubwa,” alisema Sadiki.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mbaraka Ally alisema wakulima hao wameingia ubia na Mfuko wa Pensheni wa LAPF ili kuweka mitambo mikubwa zaidi itakayokidhi uzalishaji wa zao hilo.

Alisema wakulima wamekuwa wakizalisha tani 15 kwa mwaka lakini kwa sasa uzalishaji utaongezeka kutokana na mtambo mpya kuwa na uwezo wa kusaga tani 20 za tangawizi mbichi kwa siku.