RC awataka waliojenga jirani na jeshi waondoke, meja JKT asisitiza elimu

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo

Muktasari:

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema hayo akiongeza kuwa maeneo yote ya wazi yanayomilikiwa na majeshi si kwamba hayana kazi au yameachwa bure, bali yapo mahsusi kwa ajili ya masilahi mapana ya kijeshi.

Kibaha. Wananchi wanaoishi kando ya makambi ya jeshi wakiwamo wale waliopo jirani na kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu, wametakiwa kuondoka mara moja na kuacha kupimana nguvu na askari kwa kuwa wao hawajui siasa, badala yake wanafuata sheria.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema hayo akiongeza kuwa maeneo yote ya wazi yanayomilikiwa na majeshi si kwamba hayana kazi au yameachwa bure, bali yapo mahsusi kwa ajili ya masilahi mapana ya kijeshi.

Ndikilo alisema hayo juzi katika sherehe za kufunga mafunzo ya ulinzi kwa vijana 529 wa Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (Suma JKT) kundi la saba yaliyohitimishwa katika viwanja vya Ruvu JKT Mlandizi wilayani hapa. “Pamoja na kufunga mafunzo haya naomba nifikishe ujumbe kwa wananchi wote wa mkoa kuwa, waache kutamani maeneo ya wazi ya majeshi maana yapo mahsusi kwa shughuli mbalimbali za jeshi na ulinzi wa Taifa, kwa hiyo mliopo kandokando muondoke, msitake kupimana mabavu au nguvu na hawa jamaa,” alisema.

Kaimu mkuu wa Kikosi cha Ruvu JKT, Meja Festo Mbanga alieleza kuwa wataendelea kuwaelimisha wananchi kutambua umuhimu wa kukaa mbali na maeneo ya jeshi na wasipofuata ushauri huo, basi watatumia sheria ili kuendeleza uhusiano mwema na jamii inayozunguka maeneo hayo.

Awali, mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Suma JKT Ltd, Meja Alfred Mwaijande alisema vijana hao walianza mafunzo Agosti wakiwa 538 na wamehitimu 529.