RCO atoa ushahidi kesi ya Sugu

Muktasari:

Shahidi Chambu ameiambia Mahakama hiyo leo Februari 9  kwamba shahidi wa tatu na wanne ambao ni maofisa wa polisi katika ofisi yake walimpa taarifa hizo kwamba Sugu na Masonga wametoa maneno hayo.


Mbeya. Shahidi wa tatu upande wa utetezi katika kesi inayowakabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel  Masonga, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, (RCO) Modestus Chambu  ameiambia Mahakama Hakimu Mkazi-Mbeya kuwa  alipokea taarifa za watuhumiwa hao za  kutamka maneno ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Shahidi Chambu ameiambia Mahakama hiyo leo Februari 9  kwamba shahidi wa tatu na wanne ambao ni maofisa wa polisi katika ofisi yake walimpa taarifa hizo kwamba Sugu na Masonga wametoa maneno hayo.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amemuuliza  swali shahidi huyo kwamba askari hao aliwatuma kufanya nini kwenye mkutano huo, shahidi huyo amedai kwamba: “Mimi ni RCO  wa Mkoa, ninao wajibu kuchunguza na kufuatilia  usalama na amani eneo lolote hivyo niliwatuma kwenda kuchunguza kama kuna lolote kuhusu  uvunjifu wa amani.”

 Shahidi Chambu alipoulizwa na Kibatala kama baada ya kuambiwa washtakiwa hao wametenda kosa alichukua hatua ya kuwakamata, amedai siku hiyo hakufanya hivyo kwa sababu za kiusalama zaidi.

Amedai kuwa alitumia njia ya kumpigia simu Sugu kwamba anamhitaji ofisini kwake kwa ajili ya mahojiano akiwa na Masonga na walipofika ofisini kwake akaweka chini ya ulinzi.

“ Desemba 31 mwaka jana, nilimpigia simu Sugu kwamba ninamhitaji kwa mahojiano siku iliyofuata, ila akaniomba kwamba siku iliyofuata ilikuwa sikukuu hivyo tukakubaliana kukutana Januari 2, 2018 na walipofika ndiyo 'nikawa-arrest,'' amesema.

Baada ya Wakili Kibatala kumaliza kumwongoza shahidi wake Chambu, Wakili wa Serikali, Joseph Pande alisimama na kuanza kumuuliza maswali kadhaa.

Wakili Pande alimuuliza shahidi huyo wa utetezi kwamba: “Unafikiri maneno yaliyotamkwa na washtakiwa hao yalikuwa na maana gani?”

Shahidi Chambu alijibu: “Bila kupapasa macho maneno haya ni ya fedheha, udhalilishaji dhidi ya Rais wa nchi na kwa wananchi.”

Shahidi wa nne wa utetezi, Grace Malya ambaye ni mke wa mshtakiwa wa pili (Masonga), amedai mahakamani hapo kwamba muda uliotajwa kufanyika mkutano huo, mumewe alikuwa naye nyumbani kwao Nsalaga-Uyole jijini Mbeya akimhudumia  kwa vile alikuwa anaumwa.

“Asubuhi mume wangu alikwenda kazini kwake, na ilipofika saa saba mchana nilimpigia simu nikimtaka arudi nyumbani ninaumwa, hivyo ilichukua takribani dakika 45 kufika nyumbani, akanihudumia tatizo langu na baada ya hapo aliendelea kunitazamia hali yangu, hakutoka kwenda popote na hata siku iliyofuata alishinda nyumbani tu kwa ajili ya kuupokea mwaka mpya,” amedai.

Shahidi wa tano wa utetezi, Boid Mwabulanga  ameiambia Mahakama kuwa maneno yanayodaiwa kutamkwa na Sugu kwenye mkutano huo, hakuyasikia na badala yake amesikia  mahakamani hapo huku akisisitiza kwamba mshtakiwa wa Pili (Masonga) hakumuona katika mkutano huo.

Wakili Kibatala alimtaka kuthibitisha kama Masonga alikuwapo au hakuwapo siku hiyo mkutanoni ambapo shahidi huyo alitamka: “Huyo Masonga kwenye mkutano ule sikumuona, kwanza ndiyo nashangaa hapa kusikia hivyo.”

Shahidi wa sita, Mdude Nyagali ameiambia  Mahakama hiyo kwamba alikuwapo kwenye mkutano huo na hakusikia Mbunge Sugu akitamka maneno hayo.

Na kuhusu  tuhuma zinazomkabili Masonga kutamka maneno hayo, Shahidi huyo aliiambia Mahakama hiyo kwamba anashangaa, siku hiyo alikuwa naye ofisini lakini ilipofika saa saba hivi mchana alipigiwa simu na mke wake, akasema anamhitaji nyumbani kwani  mke wake anaumwa .

 Hivyo akaondoka kwenda nyumbani kwake, na hata ilipofika muda wa mkutano, nilimpigia simu ili twende naye  lakini hakupokea simu yangu na hakuonekana mkutanoni. Hivyo hizi habari za kutamka maneno haya labda kama alizungumzia nyumbani kwake.

Hata hivyo, wakati Wakili Kibatala akimwongoza shahidi wake huyo, kuliibuka  mzozo wa mawakili baina ya Kibatala na Wakili wa Serikali Pande kwamba, Kibatala anatumia muda mwingi kuzungumza huku akiiambia Mahakama kwamba wakili huyo ni mwanasiasa hivyo hatamaliza kwa muda.

Kitendo hicho kilionekana kumkwaza, Kibatala na kumtaka Wakili Pande kumuomba radhi kwani si mwanachama wa chama chochote cha siasa na tofauti na hapo ataje ni mwanachama wa chama gani.

Wakili Pande ameendelea kusimamia msimamo wake kwamba Kibatala ni mwanachama wa Chadema na kama anataka athibitishe basi ampe miezi miwili kufanya hivyo.

Kutokana na mvutano huo, Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Michael Mteite aliamua kuiahirisha mahakama kwa muda ili kwenda kuwasuluhisha  ofisini kwake.