Wednesday, January 11, 2017

RPC: Chondechonde wapigadebe tusaidieni

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari 

By Hawa Mathias, Mwananchi hmathias@mwananchi.co.tz

Mbeya. Polisi mkoani hapa imewahamasisha waendesha bodaboda na wapigadebe kushirikiana nao ili kuukomesha mtandao wa biashara za kulevya ulipo stendi kuu ya mabasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari amesema hayo wakati akitoa taarifa  mbele Mkuu wa mkoa huo, Amos Makala aliyekuwa akikabidhi pikipiki mbili za kuzoa taka kwa diwani wa Sisimba, Geofrey Kajigili.

“Nina taarifa za kutosha, kifuatacho ni utekelezaji, tunahitaji ushirikiano kutoka kwenu wapigadebe na wananchi mnaotumia kituo hiki,” amesema.

Pia, amesema hawatashindwa na watu wachache huku akiwatahadharisha wafanyabishara hao  kuwa watafute sehemu nyingine ya kwenda kufanyia biashara hiyo haramu na siyo Mbeya.

“Amani ya nchi inapatikana kwa wananchi wenyewe, kufuga wahalifu siyo jambo jema, wafichueni ili mfanye shughuli zenu kwa usalama,” alisema.

Diwani Kajigilia amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanya kazi kwa makini na kurejesha hali ya usalama Mbeya.

 

-->