Friday, September 21, 2018

Raia wa Malawi kizimbani akidaiwa kuishi nchini bila kubali

 

By Taus Ally , Mwananchi tally@ Mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Raia wa Malawi, Edward Banda (38) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuwapo nchini bila kibali, kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Serikali na kujipatia kitambulisho cha mpiga kura kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo leo Septemba 21,2018 amesomewa mashtaka hayo na wakili wa Serikali Mwandamizi, Veronika Matikila mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wanjah Hamza.

Wakili Matikila amedai Septemba 18, 2018 katika kituo cha daladala eneo la Kawe Wilaya ya Kinondoni  alikutwa akiwa hana nyaraka za kumuwezesha kuwapo nchini.

Amedai mshtakiwa huyo, kati ya Januari na Oktoba 2015 katika shule ya msingi Mbezi Beach Dar es Salaam alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuwa yeye ni Mtanzania ili aweze kupata kitambulisho cha mpiga kura.

Iliendelea kudai mshtakiwa huyo, katika kipindi hicho cha kati ya Januari na Oktoba 2015, katika Shule ya Msingi ya Mbezi Beach kwa udanganyifu aliwadanganya maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi waweze kumuamini na kumpatia kadi ya mpiga kura namba 1-1001-8940-587-6.

Baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kuzungumza chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Hata hivyo, wakili huyo aliwasilisha hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mahakamani hapo ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo.

Baada ya mshtakiwa huyo kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

-->