Raila aiomba Marekani kumaliza mkwamo wa kisiasa Kenya

Muktasari:

Juhudi za wajumbe wenu hazijafanikiwa mpaka sasa kuzima mgogoro na hebu niseme wazi Kwa namna Fulani wamechangia katika mgogoro huu.

 

Nairobi, Kenya. Kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga jana aliwaomba washirika wa maendeleo wa kimataifa wa Kenya kujihusisha kikamilifu kusaidia kumaliza mkwamo wa kisiasa nchini.

Katika hotuba yake ya dakika 30 akiwa jijini Washington, DC, Marekani Odinga amezitaka nchi za Magharibi kuchukua hatua akisema wanadiplomasia wan chi hizo wamejikita zaidi kukabiliana na kukua kwa siasa kali na ugaidi huku wakipuuza ufinyu wa demokrasia katika mgogoro juu ya uchaguzi wa rais mwaka huu.

“Nimekuja huku Washington kuwaletea ujumbe rahisi: Tunahitaji mshiriki kwa nguvu na kutumia mikono mingi iliyonayo serikali yenu ili kuwasaidia wajumbe wenu walioko Nairobi,” alisema katika Kituo cha Usalama na Mafunzo ya Kimataifa.

“Juhudi za wajumbe wenu hazijafanikiwa mpaka sasa kuzima mgogoro na hebu niseme wazi: Kwa namna Fulani wamechangia katika mgogoro huu,” alisema na akazishutumu nchi za magharibi kwa kuiacha Kenya ielekea njia ya utawala wa mtu mmoja na udikteta.

“Mgogoro wa sasa wa Kenya kuhusu uchaguzi haujachochewa na wizi wa wazi wa kura kwa mara ya tatu pekee...Hebu niweke sawa: Kenya inapiga hatua kuelekea kuwa nchi ya kidikteta,” alisema.

“Serikali ya Jubilee imepora mamlaka ya kila taasisi ili kufanikisha lengo la kulidhibiti taifa au walivyojitangazia kutawala hadi mwaka 2032,” alisema Odinga na akaongeza kwamba anaamini Kenya inahitaji uchaguzi mpya na wa kuaminika.