Raila Odinga ajiondoa kugombea urais

Muktasari:

  • Kwamba baada ya kufikiria sana juu ya nafasi yao kuhusiana na uchaguzi wa marudio na kwa kuangalia maslahi mapana ya watu wa Kenya, ukanda na ulimwengu kwa ujumla, wameona bora Nasa wajiondoe kugombea.

Nairobi, Kenya. Mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani cha National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga amejiondoa katika uchaguzi wa marudio uliopangwa Oktoba 26.

Katika uamuzi uliotangazwa mchana leo, Odinga amesema pia kwamba mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka hatashiriki uchaguzi huo.

“Baada ya kufikiria sana juu ya nafasi yetu kuhusiana na uchaguzi wa marudio na kwa kuangalia maslahi mapana ya watu wa Kenya, ukanda na ulimwengu kwa ujumla, tunaamini kwamba ni bora Nasa tujiondoe kugombea uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26, 2017,” amesema Odinga.

Odinga amesema Nasa imekuwa ikitoa wito uchaguzi uwe huru na wa haki kwa kuzingatia matakwa ya Katiba lakini hakuna mwitiko mwema.

“Tumefikia hitimisho kwamba hakuna nia njema kutoka (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) IEBC kuhakikisha kwamba dosari na ukiukwaji wa sheria ulioshuhudiwa kabla hautajitokeza tena,” amesema.

Ameishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa “kupiga mawe” maamuzi ya kuwa na uchaguzi wa marudio wa kuaminika.

“Tumefikia uamuzi wa mwisho kwamba hakuna nia njema kwa upande wa IEBC kufanya mabadiliko yoyote katika shughuli zao na watumishi kuhakikisha kwamba ‘dosari na kasoro’ zilizosababisha uchaguzi wa Agosti 8, 2017kubatilishwa hazitajirudia tena.”

“Dalili zote zinaonyesha kwamba uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26 utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa awali,” amesema.

Alimgeukia Rais Uhuru Kenyatta na chama chake cha Jubilee kwa kushinikiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi akisema hatua hiyo inaonyesha kwamba hakuna nia njema ya ushindani katika uwanja uliosawa.

“Uchaguzi pekee ambao utawala wa Jubilee inapendelea ni ule ambao wao lazima washinde hata kama ni kwa kukiuka sheria,” amesema.

Amewashuku Rais Kenyatta na makamu wake William Ruto kwa kujigamba kwamba wana wingi wa watu katika Bunge la Taifa na Seneti akisema viongozi wawili hawa “wanakusudia kupindua utaratibu huu mpya na kuurejesha wa zamani.”