Kanisa, wafanyabiashara wamtatiza Raila

Muktasari:

Ofisa mmoja kutoka Kaunti ya Nairobi alisema wamepokea maombi mawili wakitaka kutumia Uhuru Park Januari 30, tarehe iliyopangwa pia kwa Odinga kuapishwa.

Nairobi, Kenya. Kanisa na kikundi kimoja kilichojiita Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Nairobi vimeomba kutumia uwanja wa jiji wa Uhuru Park Januri 30, eneo ambalo muungano wa upinzani wa Nasa kwa sherehe za kuapishwa Raila Odinga kuwa rais wa watu.

Utata huo umeibuka wakati Odinga na vinara wenzake Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi wakizidisha presha dhidi ya serikali ya Jubilee ikubali mjadala wakiapa kwamba wataendelea na mipango yao ikiwa Rais Uhuru Kenyatta hatakubali kufanya mazungumzo nao wiki hii.

Pia walitumia uzinduzi wa Baraza la Watu Mombasa kwenye viwanja vya Uhuru Gardens kuyaonya mataifa ya Magharibi kuacha kujiingiza katika masuala yao.

Ofisa mmoja kutoka Kaunti ya Nairobi alisema wamepokea maombi mawili wakitaka kutumia Uhuru Park Januari 30, tarehe iliyopangwa pia kwa Odinga kuapishwa. Alisema kanisa na jumuiya ya wafanyabiashara wanatakiwa kulipa fedha ili waweze kupewa eneo hilo kabla ya mkutano wao.

“Tumepokea maombi mawili kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Nairobi na kanisa na tunatarajia malipo yatafanyika Jumatatu,” alisema ofisa huyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara waNairobi, Wilfred Kamau alisema walipewa idhini ya kuendelea na mipango yao na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuandaa kambi ya matibabu Uhuru Park Januari 30.

Kamau alisema kambi hiyo imelenga kuwasaidia vijana wa mitaani ili wafanyiwe tohara na kwamba matibabu yao yatakuwa bure.

“Tumeiandikia barua Serikali ya Kaunti na tunatakiwa kesho Januari 22 (leo) kulipa Sh250,000 ili turuhusiwe kuutumia uwanja. Nasa itabidi watafute uwanja mwingine ikiwa watataka kusonga mbele na tukio lao. Tutatumia Uhuru Park siku hiyo,” alieleza Kamau alipoulizwa kwa njia ya simu.

 

Msisitizo wa Nasa

Katika mkutano wao wa Mombasa mwishoni mwa wiki, viongozi wa Nasa walisisitiza kuwa walishinda uchaguzi wa Agosti 8, 2017 lakini ushindi wao uliporwa akapewa Rais Kenyatta na makamu wake William Ruto. Walisema sherehe za kiapo zilipata Baraka kutoka kaunti sita za Pwani.