Rais Kenyatta aelekea kumstaafisha Odinga

Wafuasi wa mgombea urais wa Kenya, Raila Odinga wakiandamana katika eneo la Mathare jijini Nairobi nchini humo jana wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyokuwa yakitangazwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Picha na AFP.

Muktasari:

Wakati wa kampeni alitangaza kuwa akishindwa safari hii itakuwa mara yake ya mwisho kugombea urais.

Mgombea urais wa muungano wa upinzani wa Nasa, Raila Odinga (77) alipoibuka juzi usiku kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyokuwa yanaelekea kumpa ushindi Rais Uhuru Kenyatta (55), ilikuwa ni ishara mbaya kwake na wanasiasa wa Tanzania wamezungumzia walichojifunza.

Baadhi ya wasomi na wanasiasa waliozungumza na Mwananchi jana walisema kuna mambo matano ya kujifunza kutoka Uchaguzi Mkuu wa Kenya ikiwamo Serikali kuruhusu wafungwa na Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuanza kupiga kura.

Mambo mengine ya kujifunza ni kuwapo kwa nafasi ya mgombea binafsi, ushindani wa hoja pamoja na mwamko mkubwa wa Wakenya kujitokeza kupiga kura ikilinganishwa na hapa nchini.

Odinga akataa matokeo

Hata hivyo, Odinga aliwaambia wanahabari kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake bila kufuata utaratibu, kwamba kabla ya matokeo yoyote kutangazwa, IEBC ilitakiwa kuwapa mawakala wa vyama vya siasa Fomu 34A kutoka vituoni.

“Mfumo umeacha kufanya kazi. Sasa ni mitambo inayopiga kura. IEBC wamesema kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu 34A pekee zinazoonyesha chanzo cha matokeo,” alisema.

“Kwa hivyo, tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka IEBC itoe fomu 34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa.”

Baadaye Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati aliwaambia waandishi wa habari kwamba matokeo hayo yanayotangazwa kutoka jengo la Bomas bado ni ya awali.

“Kashfa zinazotolewa na baadhi ya wadau dhidi ya utangazaji wa matokeo si sahihi. Tunapenda kuwaarifu kwamba matokeo yanayoonekana kwenye skrini za IEBC siyo ya mwisho,” alisema Chebukati.

Chebukati alisema matokeo rasmi na ya mwisho ni yale yaliyomo kwenye Fomu 34A na 34B kutoka kwenye vituo na majimboni. Baadaye jana mchana, Odinga alisema wamepata habari kwamba mitambo ya Tume ilidukuliwa na matokeo halisi kufanyiwa ukarabati.

Madai hayo hayakuizuia IEBC kuendelea kutangaza matokeo ya awali ya urais mtandaoni na hadi saa 1.42 usiku, Rais Uhuru wa chama cha Jubilee alikuwa mbele kwa kura 7,989,006 sawa na asilimia 54.32 akifuatiwa na Odinga aliyekuwa na kura 6,589,395 sawa na asilimia 44.8. Vituo vilivyokuwa vimewasilisha matokeo ni 39,507 kati ya 40,883. Hata hivyo, jana usiku tume hiyo ilianza kuhakiki fomu hizo.

Ikiwa matokeo hayo hayatabadilika, huenda ahadi aliyoitoa Odinga wakati wa kampeni kwamba “Hii itakuwa vita yake ya mwisho ya urais” ikatimia. Uhuru alisema akishindwa atabaki katika siasa.

Ashinda nje ya nchi, wafungwa

Pamoja na kuwa nyuma kwa tofauti ya asilimia 10, Raila alipata kura 408 dhidi ya 322 za Uhuru kwa Wakenya waishio Uganda. Raila aliongoza pia kwa kura 394 dhidi ya 393 za Uhuru nchini Tanzania, Burundi; Raila 48 na Uhuru 47. Rwanda; Uhuru aliongoza kwa 298 na Raila 255, na Afrika Kusini; Uhuru 358 na Raila 302.

Kadhalika, kura zilizotangazwa kwa wapigakura wafungwa, Raila alipata kura 2,048 na Uhuru kura 1,710. Hata hivyo, wakati Odinga akikataa matokeo hayo mgombea binafsi Japheth Kavinga Kaluyu ambaye hadi jioni alikuwa amejikusanyia kura 11,337 sawa na asilimia 0.08 alitangaza kukubaliana na matokeo.

Kaluyu alisema amefanya tathmini ya kutosha na kubaini kwamba hakuwa na nafasi yoyote ya kumpiku Rais Uhuru aliyekuwa akiongoza.

Ghasia zaibuka

Hatua ya Odinga kukataa matokeo yaliyokuwa yakimpa ushindi Rais Uhuru ilisababisha watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wake kufanya maandamano na kuchoma matairi barabarani. Maeneo yaliyokumbwa na ghasia ni Homa Bay na Mathare jijini Nairobi na Kondele, Kisumu.

Polisi wa kuzuia ghasia walilazimika kuwatawanya waandamanaji kwa maji ya washawasha, mabomu ya kutoa machozi na maeneo mengine kufyatua risasi za moto kwa makundi ya vijana waliokuwa wakiendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya jiji la Nairobi lilikuwa tulivu kutwa nzima huku baadhi maduka na ofisi hasa za binafsi zikiwa zimefungwa na pilikapilika za mitaani zikiwa za kiwango cha chini tofauti na ilivyozoeleka.

Juzi siku ya uchaguzi, barabara za jiji la Nairobi zilikuwa tupu, lakini jana watu waliongezeka kiasi na magari pia yalikuwa ya kuhesabu.

Mwandishi wa NTV aliyeko kwenye kituo hicho cha Bomas yanapotangazwa na matokeo hayo, aliripoti kwamba kufikia jioni jana mashabiki wa Jubilee walikuwa wamejazana katika eneo hilo. Japokuwa wengi wao walionekana wenye nyuso zenye furaha, hawakutaka kusema lolote hadi IEBC itangaze matokeo ya mwisho.

Maoni ya Watanzania

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema: “Ukiruhusu Watanzania walioko nje kuanza kupiga kura itasaidia Taifa kuwa na takwimu sahihi ya Watanzania wanaoishi katika mataifa mbalimbali duniani na wengi watajitokeza. Lakini pili, itasaidia kuongeza uzalendo kwa Watanzania hao kujiona wako sehemu ya taifa lao.”

Mrema pia alipongeza uamuzi wa Kenya kuwahusisha wafungwa na viongozi kufanya kampeni za kistaarabu. “Katika kipindi cha miezi mitatu ya kampeni, hakuna matusi miongoni mwa wagombea wa nafasi za urais kati ya Odinga na Uhuru hatua iliyoimarisha usalama. Tulikuwa tunasikia ushindani wa hoja tu, Uhuru anasema atafanya nini tena na Odinga anasema kwa nini Uhuru hawezi, tena siyo kama kwetu huku mara utasikia sijui nani mgonjwa, tujifunze hilo wanasiasa wa Tanzania,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii, Renatus Muabhi alisema ukomavu wa kidemokrasia umeonekana kwa wapigakura wa nchi hiyo ikilinganishwa na Tanzania, jinsi walivyojitokeza kupiga kura kwa wingi ili kuamua hatima ya maisha yao.

Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ali alisema, “Yako masuala ya kujifunza mengi ila vizuri kuangalia utamaduni na historia yake (kwa hayo mazuri) kwa nini yanaweza kufanya vizuri zaidi huko lakini yasifanye vizuri katika mfumo wa taifa lingine, malengo yanaweza kuwa sawa ila tatizo likajitokeza kwenye mifumo ya uendeshaji wake.”