Rais Maduro ashinda kwa kishindo Venezuela

Muktasari:

Asilimia 46.01 ya watu waliokuwa wamejiandikisha ndio walipiga kura chini ya matarajio ya asilimia 48 ambapo watu 8.6 milioni walipiga kura.

Venezuela. Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro Jumapili aliibuka mshindi wa muhula mwingine wa miaka sita, baraza la uchaguzi limetangaza matokeo hayo yanayoonekana ya utata.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Rais wa Baraza la Taifa la Uchaguzi (CNE), Tibisay Lucena, Rais Maduro alipata kura milioni 5.8 wakati mpinzani wake mkuu, Henri Falcon aliambulia kura milioni 1.8.
Asilimia 46.01 ya watu waliokuwa wamejiandikisha ndiyo waliopiga kura chini ya matarajio ya asilimia 48, watu milioni 8.6  walipiga kura.
"Hii ilikuwa siku ya kihistoria! ... siku ya ushindi mzuri," alisema Maduro nje ya makazi ya rais jijini Caracas Jumapili usiku.
"Walinidharau," Maduro aliwaambia wafuasi wake waliokuwa wakishangilia kwa kupiga fashifashi.
"Haijawahi kutokea siku za nyuma mshindi wa urais akapata asilimia 68 ya kura za wananchi," alisema Maduro na kuongeza: "Sisi ni nguvu ya kihistoria iliyogeuka hali kuwa ushindi wa kudumu."
Lakini mpinzani wake, Falcon alitoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi mwingine akilalamikia kuwa uchaguzi wa Jumapili ulikuwa umejaa dosari na ukosefu wa uhalali. "Hatutambui matokeo ya uchaguzi huu kuwa halali," aliviambia vyombo vya habari na kuongeza: "Lazima ufanyike uchaguzi mwingine Venezuela."