Rais Magufuli aifumua CCM

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) wakiwa katika kikao kilichofanyika Ikulu Dar es Salaam jana na kuogozwa na Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli

Muktasari:

Mabadiliko hayo ambayo aliwasihi wajumbe wasiyaogope, yamepitishwa na katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliyoketi jana jijini Dar es Salaam chini yake.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amefanya mabadiliko makubwa katika muundo wa chama hicho kwa kupunguza idadi ya vikao na wajumbe wa ngazi zote.

Mabadiliko hayo ambayo aliwasihi wajumbe wasiyaogope, yamepitishwa na katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliyoketi jana jijini Dar es Salaam chini yake.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliyemaliza muda wake, Nape Nnauye alisema baada ya NEC kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, imeamua kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao vya chama ili kuongeza ufanisi wa utendaji na muda wa viongozi kufanya kazi za chama kwa umma badala ya kutumia muda mwingi vikaoni.

Katika mabadiliko hayo, wajumbe wa Halmashauri Kuu wamepunguzwa kutoka 388 hadi 158. Pia kikao hicho kimepunguza idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kutoka 34 hadi 24.

Mbali na wajumbe wanaoingia CC kutokana na nyadhifa zao, kutakuwa na wajumbe watatu wa kuchaguliwa na NEC kutoka bara na watatu kutoka Zanzibar.

Awali, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho Kamati Kuu ilikuwa inaundwa na wajumbe wasiozidi 14 waliochaguliwa na NEC wakiwemo wanawake wasiopungua wanne, wawili kutoka Bara na wawili Zanzibar. Pia, wajumbe wa heshima wasiozidi watano ambao walipendekezwa na mwenyekiti wa CCM kutokana na uongozi wao uliotukuka.

 

Kupunguzwa vikao

Kuhusu vikao vya kawaida vya NEC, Nape alisema vitakuwa vikifanyika kila baada ya miezi sita badala ya minne ya awali, isipokuwa maalumu inapohitajika.

“Vikao vya kawaida vya Kamati Kuu vitapunguzwa ili vifanyike kila baada ya miezi minne badala ya miezi miwili isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.”

Alisema kwa ngazi ya mkoa, wajumbe wa kamati za siasa watapunguzwa kwa kuondoa watatu ambao ni katibu wa uchumi na fedha na nafasi mbili za wajumbe wa kuchaguliwa na halmashauri za mikoa,” alisema Nape.

Kuhusu vikao vya kawaida vya kamati ya siasa ya mkoa, alisema vitafanyika kila baada ya miezi mitatu badala ya kila mwezi kama ilivyo sasa isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.

Kwa upande wa wilaya, alisema wajumbe wa kamati ya siasa watapunguzwa kwa kuwoandoa katibu wa uchumi na fedha, katibu wa kamati ya madiwani na wajumbe wawili wa kuchaguliwa na halmashauri na jumla yao watakuwa wanne.

“Vikao vya kawaida vya kamati ya siasa ya wilaya vifanyike kila baada ya miezi mitatu badala ya kila mwezi isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.

 

Muundo wa chama

Kuhusu muundo wa wilaya za chama, Nape alisema NEC imeufanya uendane na muundo wa sasa wa Serikali na kwamba idadi ya wanachama kuanzisha shina sasa itaanzia wanachama 50 hadi 300 na ile ya kuanzisha tawi itakuwa kuanzia 301 hadi 1,000.

Hata hivyo, Nape alisema idadi hiyo izingatie eneo la kijiografia na wingi wa wanachama katika eneo hilo.

“Vikao vya kawaida vya kamati za siasa za ngazi hizi viwe vinafanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu,” alisema.

Kuhusu nafasi za uongozi, alisema mwanachama anatakiwa kuwa na nafasi moja tu ya uongozi wa kazi za muda wote kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi wa CCM, Toleo la 2012, Kifungu cha 22 na 23.

Alizitaja nafasi hizo kuwa ni mwenyekiti wa tawi, kijiji au mitaa, kata/wadi, jimbo, wilaya na mkoa.

Wengine ni makatibu wa halmashauri kuu wa ngazi zote zinazohusika pia, mbunge, mwakilishi na diwani.

Kuhusu vyeo ambavyo haviko kwenye katiba, Nape alisema haviruhusiwi katika chama au jumuiya zake.

“Kwa mfano umoja wa makundi mbalimbali kama wenyeviti wa ngazi mbalimbali (mfano: mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM), makamanda (UVCCM), washauri (UWT) na walezi (Wazazi) katika ngazi zote,” alisema.

 

Uhakiki wa wanachama

Wakati chama hicho kikijinadi kuwa na wanachama zaidi ya milioni nane, Nape alisema NEC imeona ipo haja ya kufanya uhakiki ili kujua idadi sahihi, huku pia matumizi ya kadi za kielektroniki yakianzishwa.

Alisema kadi hizo mpya zitadhibiti usahihi na kuondoa wanachama hewa huku kadi za jumuiya za UWT, wazazi na UVCCM zikifutwa na kubakiza kadi moja tu ya uanachama.

Kuhusu uendeshaji wa jumuiya za chama na mali zake, alisema utakuwa chini ya usimamizi wa Baraza la Wadhamini.

“Makatibu wakuu wa jumuiya watakuwa wanateuliwa na Kamati Kuu na naibu makatibu wakuu watateuliwa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa,” alisema.

Mbali na mabadiliko hayo, Nape alisema NEC pia imeamua kufanya mabadiliko kwenye bendera na nembo zake ili ziwe na mwonekano mzuri zaidi, japo zitabaki hivyohivyo.

Kuhusu utumishi katika chama, alisema nafasi za makatibu wasaidizi wa mikoa na wilaya zitaondolewa na badala yake kazi zao zitatekelezwa na makatibu wa jumuiya za chama wa mikoa na wilaya kwa utaratibu utakaopangwa.

 

Uchaguzi wa Zanzibar

Kuhusu uchaguzi wa Zanzibar uliofutwa Oktoba 25, 2015 na kurudiwa Machi 20, Nape alisema NEC imeagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya kufanya tathmini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.

“Tuliwapa kazi wenzetu wa Zanzibar kufanya tathmini ya uchaguzi sasa wameleta, nadhani kuna vitu havijakaa sawa, sasa tunawarudisha tena na tunatuma timu iende ikaweke sawa,” alisema.

Kuhusu wasaliti wa chama, Nape alisema: “Mwenyekiti wa kamati ya udhibiti na nidhamu ametakiwa akamilishe kazi ya taarifa ya udhibiti kwa wanachama waliokiuka mienendo ya kiuanachama kabla ya kuanza uchaguzi mkuu wa chama Februari 2017, mikoa na wilaya ambazo hazijaleta taarifa zao za kiudhibiti ziwe zimefikisha taarifa zao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Udhibiti na Nidhamu kabla ya Januari 30, 2017.”

 

Uteuzi

Mbali na hatua hizo, Rais Magufuli amemteua Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Nape ambaye sasa ni Waziri wa Habari huku Rodrick Mpogolo akichukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) iliyoachwa wazi na Rajabu Luhwavi aliyeteuliwa kuwa balozi.

Mwingine ni Kanali Ngemela Lubinga aliyekuwa msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambaye ameteuliwa kuwa Katibu NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk Asha-Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Balozi.