Rais Magufuli amwapisha bosi mpya wa Takukuru

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Kamishna Diwani Athuman Msuya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa TAKUKURU katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma

Muktasari:

  • Rais Magufuli p amewaapisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk Jingu naBalozi wa Tanzania, Uganda Dk Aziz Mlima katika Ikulu ndogo ya Chamwino, Dodoma.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemwapisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Diwani Athuman leo Septemba 12.

Pia, Rais Magufuli amemuapisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk John Jingu na Balozi wa Tanzania, Uganda, Dk Aziz Polnary Mlima.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria hafla hiyo ya uapisho, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Miongoni mwao ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge, Job Ndugai na Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi.

Rais amemtaka Mkurugenzi mpya wa Takukuru CP Diwani kuungalia upya muundo wa Takukuru ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, na kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.

 

“Nataka ukaisafishe TAKUKURU, kuna baadhi ya wafanyakazi wa TAKUKURU wanajihusisha na rushwa, kawaondoe, nataka kuona TAKUKURU inashughulikia rushwa kwelikweli hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana, na tatizo kubwa ni rushwa” amesisitiza Rais Magufuli.

Pia alimtaka alimtaka kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini na kuhakikisha wanaokabiliwa  na tuhuma za kujihusisha na rushwa wanafikishwa mahakamani

Rais alimpa maagizo Dk Jingu, akimtaka kushirikiana na viongozi wengine wa Wizara ya Afya, kufuatilia usajili na utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s).

“Hakikisha haya mashirika yanafanya kazi kwa kuzingatia sheria ambazo pamoja na mambo mengine sheria zinayataka kuendesha shughuli zao kwa uwazi hasa katika masuala ya mapato na matumizi ya fedha za ufadhili wa shughuli zake,” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wa Balozi wa Uganda, Dk Mlima, Rais alimtaka kusimamia vizuri ushirikiano wa Tanzania na Uganda hasa katika baishara na uwekezaji unaoendelea kati ya nchi hizo mbili.