Rais Magufuli apigilia msumari mradi wa stempu

Rais John Magufuli akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wakati wa hafla ya kupokea gawio la Serikali kutoka Shirika la Simu Tanzania (TTCL) jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Amesema hiyo ni kwa sababu Shirika la Simu Tanzania (TTCL), linalomilikiwa na Serikali, litakuwa limeshajiandaa kuweza kutoa huduma hiyo na kusambaa nchi nzima.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema kampuni ya kigeni iliyo na jukumu la kuendesha mradi wa stempu za kielektroniki (ETS), haitaweza kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.

Amesema hiyo ni kwa sababu Shirika la Simu Tanzania (TTCL), linalomilikiwa na Serikali, litakuwa limeshajiandaa kuweza kutoa huduma hiyo na kusambaa nchi nzima.

Kauli hiyo inaweza kuwa imeweka ukomo katika mjadala ulioanza kushika kasi ndani na nje ya Bunge kuhusu uamuzi wa Serikali kuipa Societe Industrielle de Produits Alimentaire (Sicpa), zabuni ya kuweka stempu hizo za kielektroniki katika bidhaa kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato (TRA).

Wengi wanadai zabuni hiyo ilitolewa bila ya ushindani na kwamba mradi huo utaongeza gharama za uzalishaji wa bidhaa za ndani na hivyo kuzifanya zisiweze kushindana sokoni, huku Kamati ya Bunge ya Bajeti ikihofu kuwepo na ufisadi katika kuipa Scipa zabuni hiyo.

Kamati ya Bunge ilisema kampuni hiyo itawekeza takriban Sh48 bilioni, lakini itakuwa ikipata Sh65 bilioni kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano. Lakini, kwa Rais Magufuli, hilo sasa halitawezekana.

Rais Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati bungeni kukiibuliwa hoja kuhusu kampuni iliyopewa kazi ya kutekeleza mradi wa stempu za kielektroniki.

Akizungumza wakati akipokea gawio la Sh1.5 bilioni kutoka TTCL jana, Rais Magufuli alisema Serikali ilikuwa inatafuta mtu atakayeweza kukusanya kodi kwa njia ya kielektroniki kwa kuweka stempu kwenye bidhaa.

“Najua (TTCL) mnaliweza, kadri mtakavyojipanga, lakini kwa vile mlikuwa hamjawa na mtandao nchi nzima, ilibidi zitangazwe tenda na watu wengine walijitokeza,” alisema Rais Magufuli.

“Sifahamu mchakato umefikia wapi, lakini kama wapo ambao watakakuwa wameshinda, nataka niwahakikishie haitakuwa zaidi ya miaka miwili, ili kusudi ninyi muwe mmejiandaa kikamilifu,” alisema.

Alisema kwa sasa hawezi kuingilia mchakato wa zabuni na kwamba inawezekana TTCL bado haijajiandaa vizuri kuhudumia kwa mtandao ulioenea nchi nzima, lakini akalitaka shirika hilo lijiweke sawa.

“Mjipange katika direction (mwelekeo) hiyo kwamba mna opportunity (fursa) kubwa na Serikali ninayoiongoza mtapata support (mtaungwa mkono) kubwa,” alisema.

Pendekezo la kuanzisha mfumo huo lilikuwemo kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Alisema mfumo huo mpya utaanza kutumika Septemba Mosi, akitaja baadhi ya nchi ambazo zimeanza kuutumia kama Kenya, Morocco, Uturuki, Malaysia na Uswisi.

Kamati ya Bajeti

Lakini mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alisema wakati akiwasilisha maoni yao kuwa kampuni ya Sicpa ndiyo iliyoshinda zabuni hiyo na ina mkataba wa miaka mitano.

“Kamati haina pingamizi na uanzishwaji wa mfumo huu, jambo la msingi ambalo linahitaji lifanyike kwa umakini ni kujiridhisha na gharama za mfumo huo ambazo zitabebwa na watumiaji wa bidhaa,” alisema.

Ghasia alisema kamati ilifanya uchambuzi ili kubaini kiwango cha fedha ambacho Sicpa itakipata katika mkataba huo kwa mwaka mmoja ukihusisha takwimu za bidhaa tatu za maji, soda na sigara bila spiriti.

Alisema ukokotoaji unaonyesha kwa mwaka mmoja Sicpa itakusanya jumla ya Sh66.69 bilioni bila ya kuhusisha takwimu za bidhaa za spiriti.

“Kiasi hiki ni kikubwa kuliko alichowekeza katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa mkataba,” alisema Ghasia.

Kamati ilishauri mradi huo ufanywe na Serikali, akitoa mfano wa maamuzi mengine kama ya kuhamisha fedha zake kutoka benki binafsi kupeleka Benki Kuu, kuondoa ununuzi wa umeme kupitia kampuni binafsi ya MaxMalipo na ukusanyaji wa nauli za mabasi ya mwendo kasi na matumizi ya mashine za EFD.

Alisema hakuna haja ya kuipa Sicpa zabuni hiyo kwa miaka mitano, wakati mradi huo ungeweza kufanywa na Serikali yenyewe.

Mchango wa wabunge

Katika siku ya kwanza ya mjadala wa bajeti, mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu alisema alikuwa na hofu kama Serikali ilijiridhisha na mzabuni kabla ya kuingia nayo mkataba.

Alisema sehemu nyingi ambako kampuni hiyo imefanya kazi, imekuwa na matatizo kutokana na gharama zake kusababisha bei za bidhaa kupanda.

Zungu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge, alisema kampuni hiyo inachunguzwa na Bunge la Kenya na imeziangusha serikali nyingine kutokana na mfumo wake wa rushwa.

Aliiomba Serikali iipe TTCL zabuni za kutekeleza mradi huokwa kuwa ina uwezo.

Lakini mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe aliwataka wabunge wenzake kuachia Sicpa itekeleze mradi huo.

Bashe alisema wafanyabiashara wana kawaida ya kutumia mianya kukwepa kodi na Serikali imekuwa na jitihada za kuziba mianya hiyo kwa kuboresha sheria.

Alimtaka waziri kufanyia kazi mawazo yote yaliyotolewa na wabunge lakini tathimini na utendaji kazi unaonyesha kuwa maeneo ambayo kampuni ya Sicpa imewahi kufanya kazi kumekuwa na mafanikio.