NHC yatakiwa kujitathmini kwa upungufu uliopo

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu

Muktasari:

Mchechu atakiwa kuwa makini na watu anaofanya nao kazi, lakini pia kujitathmini kwa upungufu alionao.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lijisafishe na kujitathmini katika upungufu lililonao, ukiwemo wa matumizi ya fedha kabla ya kuomba mkopo serikalini.
NHC imeomba mkopo wa Sh232 bilioni kwa ajili ya kumalizia baadhi ya majengo ya ghorofa yaliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba 300 zilizojengwa na shirika hilo katika Kata ya Iyumbu mjini Dodoma leo Jumatano Desemba 13,2017,  Rais Magufuli amewataka baadhi ya wakurugenzi wa NHC kuacha kutengeneza makundi mawili kwa kuwa kufanya hivyo ni kuivunja.
Pia, amemuagiza waziri akae na bodi na kurekebisha upungufu uliopo.
“Usicheke nao, najua kona zote, michepuko yote ya humo kwa hivyo lazima mvifanyie kazi kwa ajili ya kujenga shirika hili. Niwaambie wazi, Serikali ya sasa haitoi mikopo ya ovyo mahali ambako bado kuna shaka fedha yake itatumikaje,” amesema.
Hata hivyo, Rais Magufuli amelipongeza shirika hilo kwa kusimamia miradi ya ujenzi vizuri, lakini akasisitiza matumizi ya fedha bado hayapo vizuri kutokana na bodi kutoa vibali vya ovyo.
“Ndiyo maana wakitaka kukaa vikao wanakaa nje ya nchi, wamekosa maeneo ya kukaa Tanzania nzima. Ukishaona shirika linataka kwenda kwa mwelekeo huo ni lazima uweke shaka, ndiyo maana tulikaa kimya tukazuia suala la kukopakopa maana mzigo huo utabebwa na Serikali,” amesema.
Rais Magufuli amesema Sh3.88 bilioni ambazo Serikali imezilipa kwa kununua nyumba 65 kwa ajili ya maofisa uhamiaji na wengine, zitumike kumalizia majengo.
Amesema fedha walizozitumia kununua eka 500 za ardhi mkoani Arusha wanaweza kuuza eneo hilo ili kumalizia viporo wanavyovitaka.
“Mjifunze kumeza kile kinachotosha kwenye koo. Ninayoyajua ni mengi, tuhuma zipo, hata katika majengo ya Kawe pale kuna ‘share’ ya 50/50 na mtu mwingine, mwenye share hiyo ni nani maana mimi nawajua. Ndiyo maana nataka niseme kwa dhati mjitathmini muende kwenye mlengo ninaoutaka,” amesema.
Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu na kumtaka awe makini na watu anaofanya nao kazi, lakini pia akimtaka kujitathmini katika upungufu alionao.
“Wapo watu wanaotaka ukurugenzi wako na wanawatumia mpaka wakurugenzi wa bodi kwa hiyo mnapigana vita humohumo inawezekana ndiyo maana mnashindwa kusonga mbele, wapo wanaotumiwa na wanasiasa, wanakupiga vita kwa wivu wao,” amesema.
Rais amesema, “Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo mengi vipo, unakuwa na shirika linaloshiriki na ni shirika lako, unanunua viwanja kule na wewe unanunua viwanja fulani na tukichunguza tunagundua kwamba ni yako, mkurugenzi, mwenyekiti na waziri kakaeni mkajadili mlipokosea na mtoe mapendekezo.”
Awali, Mchechu alimuomba Rais Magufuli kulipa shirika hilo kibali cha kukopa Sh232 bilioni kumalizia viporo vya miradi minne ya ujenzi katika Jiji la Dar es Salaam.
Mchechu amesema miradi hiyo yenye thamani ya Sh473 bilioni ikikamilika itawezesha shirika hilo kupata faida ya Sh118 bilioni.