Rais Magufuli ateta na Kinana Ikulu

Muktasari:

  • Vikao vya Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) vitaanza kesho Mei 28 na 29, 2018 Jijini Dar es Salaam.

Rais John Magufuli amekutana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana Ikulu, jijini Dar es Salaam, leo na kuzungumzia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa CCM.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Mei 27 imesema katika mazungumzo hayo Rais amepokea salamu kutoka kwa viongozi wa chama na Serikali wa Afrika Kusini na Zimbabwe ambako Kinana alitembelea hivi karibuni.

“Kinana aliongoza ujumbe wa viongozi wa CCM kutembelea nchi hizo na kukutana na viongozi wakuu wa vyama tawala vya ANC na ZANU-PF vinavyoongoza Serikali,” imesema taarifa hiyo

Taarifa ya Ikulu inaeleza kuwa, Kinana na Rais Magufuli wamezungumzia maandalizi ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) vitakavyofanyika kesho Mei 28 na 29, 2018 Jijini Dar es Salaam.