Rais Magufuli atoa wito EAC kusimamia rasilimali zake

Rais John Magufuli akifurahia jambo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kabla ya kuanza kwa mkutano wa 19 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Kampala nchini Uganda jana. Kushoto ni Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Rais Magufuli alisema hayo jijini Kampala jana wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa EAC unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

 Rais John Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kusimamia vyema rasilimali walizonazo na kukusanya kodi vizuri ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Rais Magufuli alisema hayo jijini Kampala jana wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa EAC unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

Katika mchango wake, Rais Magufuli alisema pamoja na kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), ni muhimu kwa Serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.

Alisema japokuwa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhari za kutosha ili kuepusha Serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na masilahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi.

“Sekta binafsi siyo mama wala baba wanakuja kufanya biashara hivyo lazima tuwe waangalifu,” alisema Magufuli.

Aliwataka wafanyabiashara kuacha kulalamika na badala yake wajitokeze kuwekeza kwenye miradi na akawakaribisha kuja Tanzania akisema kuna fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji.

“Tatizo watu wa sekta binafsi wanaongea sana... acheni kutumia mikutano kama hii kulalamika, jitokezeni mfungue uwekezaji tena Tanzania tuna maeneo mengi ambayo mnaweza kuwekeza badala ya kuendelea kulalamika,” alisema.

Kuhusu usimamizi mzuri wa rasilimali zilizopo, Dk Magufuli alitolea mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini ukiwamo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha zake baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi.

“Mimi naamini tukiamua tunaweza, nchi zetu zina rasilimali nyingi za kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Mathalani, tafiti zinaonyesha kuwa kama nchi zetu zitaweza kukusanya vizuri mapato ya kodi, zinaweza kutekeleza nusu ya miradi yake ya maendeleo.

“Lakini ukiachilia mbali mapato ya kodi, tunapoteza fedha nyingi kupitia utoroshaji wa rasilimali zetu, ripoti ya jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki imeeleza kuwa nchi za Afrika zinapoteza Dola za Marekani bilioni 150 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa rasilimali,” alisema.

Rais Magufuli leo atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Marais waliohudhuria mkutano huo ni mwenyeji, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir. Marais wa Rwanda na Burundi wamewakilishwa.

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa zamani wa jukwaa la maofisa watendaji wakuu Tanzania (CEO roundtable), Ali Mufuruki alihimiza haja ya kuboresha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.