Rais Magufuli avunja bodi ya Sumatra

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Rais amevunja bodi ya wakurugenzi wa Sumatra pamoja na ile ya ushauri ya Temesa na kuagiza uchunguzi ufanyike na wahusika waliosababisha ajali hiyo wachukuliwe hatua.

Dar es Salaam. Ndani ya saa 24 baada ya kuivunja bodi ya Temesa, Rais John Magufuli ameivunja pia bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra).

Taarifa iliyotolewa leo, Septemba 24, 2018 na kurugenzi ya mawasiliano ikulu imebainisha kuwa Rais amefanya uamuzi huo kutokana na kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere na ajali nyingine za barabarani zinazosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.

“Pamoja na hatua hiyo, kamati ya uchunguzi itakayotangazwa na Waziri Muu Kassim Majaliwa baadaye leo itaendelea na uchunguzi wa ajali ya MV Nyerere kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kama ilivyopangwa,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na kuzama kwa kivuko hicho hapo Septemba 20 katika Ziwa Victoria, jana jioni Rais alitangaza kuivunja bodi ya ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa).

Kutokana na hatua hiyo, Rais ametengua uenyekiti wa Brigedia Jenerali mstaafu Mabula Mashauri wa Temesa na Dk John Ndunguru wa Sumatra.

Taarifa zinasema kivuko hicho kilizama kikiwa na watu 265 ilhali uwezo wake ni kubeba mpaka abiria 101. Zaidi ya watu 220 wamepoteza maisha kutokana na ajali hiyo na kulazimu zaidi ya 100 kuzikwa kitaifa baada ya kutotambuliwa na ndugu zao.

Waziri mkuu pamoja na viongozi wengine wa Serikali waliongoza mazishi hayo yaliyofanyika Ukara, moja ya visiwa kilichomo katika Ziwa Victoria.