Rais Magufuli awashukuru viongozi wa dini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakishiriki kutoa sadaka katika kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano jijini Dar es salaam wakati wa  Ibada ya Jumapili kuadhimisha siku ya Bwana ya 19 baada ya Pentekoste asubuhi ya leo Septemba 25,2016.Picha zote na Ikulu

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa  Rais Magufuli amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo asubuhi ameungana na Waumini wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano lililopo Posta jijini Dar es Salaam kusali ibada ambapo amewashukuru viongozi na waumini wa kanisa hilo na madhehebu mengine ya dini hapa nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani na utulivu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa  Rais Magufuli amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.

Ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuliombea Taifa hili, ninawashukuru kwa sababu siku zote mmekuwa mkipiga magoti na kumtanguliza Mungu mbele, ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuombea amani ya nchi yetu na upendo udumu ndani yetu sisi sote.

“Makanisa yote, madhehebu yote, dini zote, vyama vyote, upendo tukiujenga ndio tutaiendeleza vizuri Tanzania yetu,” amesema Rais Magufuli.