Rais Magufuli kukutana uso kwa uso na wanahabari

Rais John Magufuli

Muktasari:

Licha ya changamoto zilizopo, Tanzania yaelezwa ni nchi nzuri

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani (WPFD) Mei 3, jijini Mwanza, wadau wa habari wamesema tasnia hiyo imefanikiwa kuwa na mchango mkubwa kuchochea maendeleo ya uchumi na jamii.

Maadhimisho hayo yatafanyika Mei 2 na kuhitimishwa Mei 3 yakiwa na kaulimbiu ‘Mawazo muhimu kwa wakati muhimu; jukumu la vyombo vya habari katika kuendeleza jamii zenye amani, haki na jumuishi.’

Akizungumza jana wakati wa maandalizi ya siku hiyo, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alitaja mafanikio kadhaa yaliyofikiwa na tasnia ya habari kuwa ni kushiriki ipasavyo katika mchakato wa Katiba Mpya mwanzo hadi ulipofikia na Uchaguzi Mkuu wa 2015 licha ya changamoto zilizojitokeza.

“Mafanikio mengine ni kuendelea kuwapo na kutekeleza majukumu yetu ipasavyo, utetezi na kudai haki zetu wakati wowote inapohitajika,” alisema Meena.

Tasnia hiyo ilikuwa mstari wa mbele kuibua na kuripoti matukio ya ubadhirifu wa fedha za umma, taarifa za ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wasiokuwa waadilifu likiwamo kulaani matukio ya vitisho, uvamizi kwa waandishi wa habari, kudhibiti na kukemea viongozi wanaoingilia na kuathiri uhuru wa vyombo vya habari.

Pamoja na mafanikio hayo, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), Jane Mihanji alisema kuna changamoto kadhaa zinazoendelea kuwakabili waandishi katika utekelezaji wa majukumu yao. Alisema kwa mujibu wa utafiti waliofanya mwaka 2015, asilimia 80 ya waandishi hawajaajiriwa.

Ofisa kutoka Wakfu wa Habari Tanzania (TMF), Radhia Mwawanga aliwataka wanahabari kuzingatia maadili na taaluma ya uandishi wa habari ili kujiepusha katika mazingira hatarishi.