Rais Mwinyi mgeni rasmi mashindano ya mtunzi bora wa mashairi

Rais mstaafu wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi 

Muktasari:

Kauli mbiu ya mwaka huu katika shindano hilo ni "Lugha Yetu, Fahari Yetu".


Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika fainali za shindano la kumpata mtunzi bora wa mashairi nchini zitakazofanyika Septemba Mosi mwaka huu.

Fainali za shindano hilo zinafanyika kwa mara ya tatu nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Meya wa jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuunga mkono juhudi ya kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na wanahabari leo Agosti 21,2018 jijini Dar es Salaam, Mratibu wa shindano hilo, Mwita Kambi amesema milango ya ushiriki itaanza leo na mwisho  ni Agosti 23, 2018.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika shindano hilo ni "Lugha Yetu, Fahari Yetu".

"Shindano litachuja na kupata washiriki kumi tu, mshindi wa kwanza atapewa zawadi ya Sh1milioni, mshindi wa pili Sh500,000 na mshindi wa tatu Sh300,000, kuanzia mshindi wa nne hadi wa 10 wanapata Sh100,000 kila mmoja, "amesema Kambi.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Kiwanda cha Mabati cha ALAF, Theresia Mmasy amesema kabla ya kufadhili shindano hilo, Kampuni ya ALAF ilionyesha dhamira ya kukuza mashindano hayo tangu mwaka 2015 kupitia wazo la mwanafasihi Ngungi wa Thiong'o.

"Ngungi alitoa wazo 2014 na tukaanza kulifanyia kazi 2015 hadi 2017 chini ya Idara ya kiswahili chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ushiriki ulikuwa kwa nchi zote zinazozungumza lugha ya kiswahili Afrika, na Salma Kikwete akiwa mgeni kama Balozi wa Kiswahili Afrika ,kwa hiyo tunaona fahari kuwa sehemu ya kukuza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi," amesema Theresia.