Rais Shein amtumia rambirambi Dk Mwinyi

Muktasari:

Askari wengine 44 walijeruhiwa na mmoja hajulikani alipo.

Dar es Salaam. Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar amemtumia rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kutokana na vifo vya wanajeshi 14.

Vifo hivyo vimetokea Desemba 7,2017 wakati wanajeshi hao wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Askari wengine 44 walijeruhiwa na mmoja hajulikani alipo.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Desemba 12,2017 na Ikulu ya Zanzibar imesema Dk Shein; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wanawakumbuka wanajeshi hao kwa ujasiri katika kuhakikisha amani inapatikana DRC na maeneo yote ya Maziwa Makuu.

Dk Shein pia ametoa rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, familia za marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Tanzania.

“Mwenyezi Mungu awape malazi mema mashujaa hao, pamoja na kuwaombea wanajeshi waliojeruhiwa wapate nafuu ya haraka na kurejea katika hali za kawaida,” amesema Dk Shein.

Miili ya wanajeshi hao 14 imerejeshwa nchini jana Jumatatu Desemba 11,2017 na imehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo.