Rais Shein mgeni rasmi tamasha la utalii Zanzibar

Muktasari:

Tamasha la utalii litafanyika kuanzia Oktoba 17 hadi 20 visiwani Zanzibar likihusisha watalii 3,000 kutoka nje ya nchi na waonyeshaji zaidi ya 150.


Dar es Salaam.  Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la utalii litakalofanyika visiwani Zanzibar kuanzia Oktoba 17 hadi 20.

Tamasha hilo litakalohusisha waonyeshaji wa masuala ya utalii zaidi ya 100 litafanyika Verde Hoteli visiwani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu tamasha hilo, Waziri wa Habari, Utalii na Urithi, Mahmoud Thabit Kombo alisema Dk Shein atafungua na atatoa zawadi kwa mshindi wa jumla siku ya kufunga maonyesho hayo.

Alisema siku hizo nne za tamasha hilo viongozi mbalimbali watakuwapo kwa nyakati tofauti, akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  Amani Abeid Karume, Rais wa Wwamu ya Nne Jakaya Kikwete na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla.

Kombo alisema wakati huu wamebadili mfumo wa kutangaza utalii wa visiwa hivyo kwa kuwataka watalii wafike wenyewe na kujionea kile wanachoambiwa.

Alisema walikuwa wakienda China, Dubai na London kutangaza utalii wa Zanzibar, lakini sasa watalii watapata fursa siyo ya kuona picha za fukwe tu, bali pia kushika mchanga halisi wa fukwe hizo.

“Mpaka sasa zaidi ya kampuni  150 zimethibitisha kushiriki huku waonyeshaji wa vitu mbalimbali 137 wamethibitisha pia uwapo wao,” alisema Kombo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Abdullah Mohammed Juma alisema utalii unakuwa siku hadi siku huku ukibadili mtizamo wa Wazanzibar.

Alisema zamani wananchi walikuwa wanaona watalii siyo sehemu ya mafanikio yao hivyo waliwaachia wawekezaji na Serikali, lakini sasa wanatambua faida wanayopata na kushiriki.

“Zamani walikuwa wakisema watalii ni haramu kwa sababu wanatembea utupu, lakini sasa baada ya kupata elimu ya kutosha wanachangamana nao ikiwa ni pamoja na kuwafundisha tamaduni za Kizanzibari.”  

“Tunakuja na utaratibu wa kuwashirikisha watalii moja kwa moja, hapo ndiyo wananchi watakuwa nao karibu zaidi kwa sababu tunataka washiriki kupika vyakula vya Kizanzibari, kuchora hina na kujifunza mambo kadha wa kadha ya visiwa hivyo,” alisema Dk Mohammed Juma.