Wednesday, February 14, 2018

Zuma ataka ANC impe sababu za kujiuzulu

 

Pretoria, Afrika Kusini. Rais Jacob Zuma jana alisema uongozi wa chama cha African National Congress (ANC) haujampatia maelezo kwa nini ajiuzulu kama mkuu wan chi.

Wakati Zuma akitoa msimamo huo mchana, asubuhi wabunge jana walipewa maelekezo ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye ikiwa ni ishara ya dhamira ya chama kuondokana na kiongozi huyo ili kuondoakana na mkwamo wa kisiasa.

“Sasa tumemtaka mnadhimu mkuu wa chama kuendelea na uwasilishaji wa hoja bungeni ya kutokuwa na Imani kesho (leo) bungeni ... ili Rais Zuma aondolewe rasmi,” alisema mweka hazina mkuu wa ANC Paul Mashatile alipozungumza na waandishi wa habari Jumatano.

Alisema bunge, ambalo lina wabunge wengi wa ANC “litasonga mbele kumchagua (Cyril) Ramaphosa kama rais wa jamhuri” - labda mapema asubuhi leo au kesho Ijumaa.

 

Mahojiano ya Zuma

Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la SABC Jumatano katika makazi yake rasmi huko Pretoria, Mahlamba Ndlofu, Zuma alisema atajiuzulu tu ikiwa uongozi wa ngazi ya juu wa ANC utamjulisha makosa aliyofanya.

“Niliuambia ujumbe wa ngazi ya juu wa watu sita kwamba kile walichoibua siyo mara ya kwanza. Waliibua mara mbili ndani ya NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa) yenyewe na hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kunieleza suala hasa ni nini. NEC wenyewe walisema ni lazima nijiuzulu, na mimi naona kuwa ni ajabu sana kwamba napaswa kufanya hivyo kwa sababu hii siyo mara ya kwanza kwamba wanasema hivi,” Zuma alimjibu mtangazaji wa SABC, Mzwandile Mbeje.

“Hili siyo suala jipya, ninahitaji kupewa maelezo kwamba nimefanya na kwa bahati mbaya hakuna mtu aliyeweza kuniambia nini nimefanya. Kuna michakato katika ANC ambayo inapaswa kufuatwa endapo nimekuwa nikifanya jambo baya,” alisema Zuma.

“Katika majadiliano, niliuliza, kwani ‘shida ilikuwa ni nini? Kwa nini nishawishiwe kujiuzulu? Je, nimefanya jambo lolote baya?’ Na kwa vyovyote viongozi waniletee hicho ambacho nimekifanya,” alisema akikana kuwa hajakataa maagizo ya chama.


-->