Rais Zuma kujibu mapigo hadharani

Muktasari:

Uamuzi wa kuzungumza na vyombo vya habari umekuja saa 24 tangu chama tawala cha African National Congress (ANC) kilipompelekea barua ya kumtaka ajiuzulu kama mkuu wa nchi.


Pretoria, Afrika Kusini. Rais Jacob Zuma anayepigwa vita katika uongozi wake anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari punde kuhusu masuala mbalimbali yanayomhusu.

Uamuzi wa kuzungumza na vyombo vya habari umekuja saa 24 tangu chama tawala cha African National Congress (ANC) kilipompelekea barua ya kumtaka ajiuzulu kama mkuu wa nchi.

Wananchi wa Afrika Kusini wanasubiri kuona iwapo Zuma atajibu uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya ANC wa kumtaka ang’atuke madarakani.

Shirika la habari la Reuters limesema halikuweza kuwasiliana na msemaji wa Zuma kwa ajili ya kupata maoni zaidi.

Wakati huohuo, ripoti zinaonyesha kwamba kikao cha Baraza la Mawaziri kimeahirishwa kutokana na mgogoro huu. Pia, msemaji wa ANC amenukuliwa akisema iwapo Zuma atashindwa kutii maagizo watatumia mbinu kali zaidi.

Mwenyekiti wa ANC, Gwede Mantashe amekaririwa akisema chama kitalazimika kutumia njia ya kumwaibisha Rais Zuma kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani, au kumshtaki na kumng’oa bungeni.

Uamuzi wa ANC

Katika mkutano wa waandishi wa habari Jumanne mchana Februari 13, 2018  kwenye makao makuu ya Luthuli, katibu mkuu wa ANC, Ace Magashule alithibitisha maofisa wa chama kumpelekea Zuma uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa kumtaka ajiuzulu.

"NEC imepokea ripoti kutoka kwa maofisa wa taifa kuhusu kikao chao na rais. NEC inajua maofisa wamekubaliana naye kimsingi ajiuzulu. Rais alipendekeza kuwa apewe muda wa miezi sita kubaki ofisini,” amesema Magashule.

 

NEC imeamua kwa mara nyingine kuzungumza na Zuma kuhus haja ya kutatua suala hili kwa haraka, lakini hakukubali likamilike katika muda mfupi. Hali hiyo ndiyo imesababisha uamuzi wa kumtaka ajiuzulu.

"Uamuzi wa NEC kumtaka mwajiriwa wake ajiuzulu umechukuliwa baada ya kumalizika njia zote za majadiliano kuhusu madhara kwa nchi kwa yeye kujiuzulu katika uongozi wa nchi, ANC na Serikali,” amesema Magashule.

Alisema chama kinamtaka Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa kuchukua majukumu ya uongozi wa nchi.

"Uamuzi wa NEC unatoa hakikisho kwa wananchi wa Afrika Kusini kipindi ambacho kuna changamoro za uchumi na  jamii ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka wa jamii,” taarifa ya NEC.