Rais akutana na Tucta

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli

Muktasari:

  • Katika Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Magufuli amesema pamoja na kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wowote utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi wenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 20 Aprili, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na wafanyakazi kwa manufaa ya Taifa.

Katika Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Magufuli amesema pamoja na kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wowote utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi wenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.

Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana nazo kama ambavyo imeanza kufanya hivyo.

“Nataka kuwahakikishia nyinyi viongozi wa TUCTA na wafanyakazi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wafanyakazi na ipo tayari kuwapigania, jambo la msingi tutangulize maslahi ya Taifa, kawaambieni wafanyakazi wachape kazi na Serikali itawalinda” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wao Viongozi wa TUCTA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Bw. Tumaini Nyamhokya wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali yake kujenga uchumi imara, kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa watumishi hewa na kulipa madeni ya watumishi.

Viongozi hao wameahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki na wajibu wa wafanyakazi na wameomba Serikali iendelee kufanyia kazi masuala mbalimbali ya wafanyakazi ikiwemo kuwalipa stahili zao na kuboresha mazingira ya kazi.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea barua yenye ujumbe wa Rais wa Jamhuri wa Rwanda Mhe. Paul Kagame iliyowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye ni Waziri wa Elimu wa Rwanda Dkt. Musafiri Papias Malimba.

Pamoja na kupokea barua hiyo, Mhe. Rais Magufuli na Dkt. Musafiri Papias Malimba wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ikiwemo katika sekta ya elimu hususani maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Rwanda kwa kuamua lugha ya Kiswahili ianze kufundishwa katika shule zake na ameahidi kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha hiyo.