Rais mpya Sierra Leone kupatikana leo

Muktasari:

  • Ili mgombea aweze kutangazwa mshindi lazima apate asilimia 55 ya kura zilizopigwa katika raundi ya kwanza, na ikiwa hakuna atakayeibuka mshindi basi itaandaliwa duru ya pili.

Freetown, Sierra Leone. Wananchi wa Sierra Leone leo watafanya uamuzi mzito kuhusu mustakabali wao watakapofika kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais atakayerithi kiti cha Ernest Bai Koroma anayemaliza muda wake.

Mbali ya rais, wengine watakaochaguliwa leo ni wabunge, mameya na maofisa wa serikali za mitaa.

Katika nafasi ya urais wamejitokeza wagombea 16 wakiwamo wanaume 14 na wanawake wawili, lakini ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya mgombea wa chama tawala cha APC, Samura Kamara na wa chama kikuu cha upinzani cha SLPP, Julius Maada Bio.

Wagombea wengine wanaopewa nafasi ya kufurukuta ni Musa Tarawally wa CDP, Samuel Sumana wa muungano wa C4C ambaye amewahi kuwa makamu wa rais wa Bai Koroma kwa vipindi viwili kabla ya kufutwa kazi kwa fedheha mwaka 2015.

Mwanamama Jemba Gbandi Ngobeh wa chama cha RUF pia anapewa nafasi ya kufanya vizuri.

Utaratibu wa kupiga ni kama ulivyo kwa nchi nyingine barani Afrika na duniani kwa ujumla kwamba wapigakura lazima wawe wamejiandikisha na wakifika kwenye vituo vya kupigia kura lazima waonyesha nyaraka muhimu au vitambulisho vinavyokubalika.

Ili mgombea aweze kutangazwa mshindi ni lazima apate asilimia 55 ya kura zilizopigwa katika raundi ya kwanza na ikiwa hakuna atakayeibuka mshindi basi itaandaliwa duru ya pili.