Ramaphosa asema ANC iliyopasuka kumtimua Zuma

Muktasari:

Kutokana na uamuzi wa Zuma mwenye umri wa miaka 75 kuwakatalia maofisa wa ngazi ya juu wa chama waliomtaka Februari 4 ajiuzulu, Kamati Kuu yenye mamlaka ya kufanya maamuzi mazito ndani ya ANC itakutana Jumatatu.

Cape Town, Afrika Kusini. Kiongozi wa chama tawala Cyril Ramaphosa alikiri Jumapili kuwa “hakuna umoja na kuna kutokubaliana" ndani ya ANC katika kipindi hiki chama kinapohaha kumtoa madarakani Rais Jacob Zuma aliyechafuka kwa kashfa.

Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 65, alisema alitaka kubadili "kipindi kigumu, ukosefu wa umoja na kutofautiana" kwa kuweka "mwanzo mpya" katika chama cha ANC, na aliapa kuukabili ufisadi ambao umeichafua Serikali ya Zuma.

Alikuwa akizungumza katika sherehe za kumbukumbu ya miaka 28 tangu Rais wa kwanza mzalendo Nelson Mandela alipoachiwa gerezani mwaka 1990.

"Tunajua mnataka jambo hili lifikie mwisho," alisema huku akishangiliwa kwa nguvu katika mkutano wa wanachama waaminifu wa chama huko Cape Town.

Kutokana na uamuzi wa Zuma mwenye umri wa miaka 75 kuwakatalia maofisa wa ngazi ya juu wa chama waliomtaka Februari 4 ajiuzulu, Kamati Kuu yenye mamlaka ya kufanya maamuzi mazito ndani ya ANC itakutana Jumatatu.

Kamati inaweza kumwondoa rais kutoka Ikulu, ingawa halazimiki kikatiba kutii amri hiyo.

"Tunajua mnataka hitimisho-tutafanya hivyo huku tukikazia macho yetu kwa lolote lenye maslahi kwa watu wetu wote," Ramaphosa, ambaye ni naibu rais wa nchi, alisema kwa sauti kubwa jana.

"Kama ambavyo mmekwishasikia, Halmashauri Kuu ya Taifa ya ANC itakutana kesho ... na kwa kuwa watu wetu wanataka suala hili lifikie mwisho, NEC itashughulikia hilo kwa usahihi."

Maelfu ya wafuasi wa ANC wakiwa wamevalia mavazi ya rangi za chama – njano, kijani na nyeusi – pia wengi wao mashati yao yakiwa na picha za Ramaphosa walihudhuria mkutano huo Cape Town katika uwanja uliotumiwa na Mandela kuhutubia mara baada ya kuachiwa gerezani. Mandela aliyetawala kipindi kimoja tu 1994 hadi 1999 alifariki dunia mwaka 2013.