Ramaphosa amfuata Zuma nyumbani

Muktasari:

Ramaphosa anapigiwa upatu kwamba anaweza kuteuliwa na Bunge kesho na kuapishwa kesho hiyo hiyo au Ijumaa.


Pretoria, Afrika Kusini. Rais wa ANC Cyril Ramaphosa amewasili kwenye makazi rasmi ya Rais Jacob Zuma leo mchana saa chache baada ya Zuma kulihutubia taifa kupitia mahojiano aliyofanya na shirika la utangazaji la SABC.

Msafara wa Ramahosa ulikuwa wa magari manane na waliwasili kwenye makazi yake rasmi ya Mahlamba Ndlopfu bila ving’ora wala taa za blu. Ajenda ya mazungumzo yao baada ya kufika haikujulikana.

Katika mahojiano na SABC, Zuma alionyesha kwamba atatoa taarifa ya maandishi baadaye leo kuhusu uamuzi wa chama chake kutaka ajiuzulu.

Ramaphosa anapigiwa upatu kwamba anaweza kuteuliwa na Bunge kesho na kuapishwa kesho hiyo hiyo au Ijumaa.

"Sasa tumemtaka mnadhimu mkuu wa chama kuendelea na uwasilishaji wa hoja bungeni ya kutokuwa na Imani kesho (leo) bungeni ... ili Rais Zuma aondolewe rasmi," alisema mweka hazina mkuu wa ANC Paul Mashatile alipozungumza na waandishi wa habari Jumatano.

Alisema bunge, ambalo lina wabunge wengi wa ANC "litasonga mbele kumchagua (Cyril) Ramaphosa kama rais wa jamhuri" - labda mapema asubuhi leo au kesho Ijumaa.

 

Mahojiano

Katika mahojiano na SABC mchana leo Rais Zuma alisema uongozi wa ANC haujampatia maelezo kwa nini ajiuzulu kama mkuu wan chi.

"Niliuambia ujumbe wa ngazi ya juu wa watu sita kwamba kile walichoibua siyo mara ya kwanza. Waliibua mara mbili ndani ya NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa) yenyewe na hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kunieleza suala hasa ni nini. NEC wenyewe walisema ni lazima nijiuzulu, na mimi naona kuwa ni ajabu sana kwamba napaswa kufanya hivyo kwa sababu hii siyo mara ya kwanza kwamba wanasema hivi," Zuma alimjibu mtangazaji wa SABC, Mzwandile Mbeje.

"Hili siyo suala jipya, ninahitaji kupewa maelezo kwamba nimefanya na kwa bahati mbaya hakuna mtu aliyeweza kuniambia nini nimefanya. Kuna michakato katika ANC ambayo inapaswa kufuatwa endapo nimekuwa nikifanya jambo baya," alisema Zuma.

"Katika majadiliano, niliuliza, kwani 'shida ilikuwa ni nini? Kwa nini nishawishiwe kujiuzulu? Je, nimefanya jambo lolote baya?' Na kwa vyovyote viongozi wanaletee hicho ambacho nimekifanya, "alisema.