Rasimu ya Katiba chungu kwa CCM

Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete (katikati) akifurahia jambo na Rais wa Zanzbar Dk Ali Mohamed Shein (Kushoto) na Katibu Mkuu wa CCM Phillip Mangula hivi karibuni mjini Dodoma

Muktasari:

  • Tayari CCM kimetangaza kufanya mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho ili kuichambua na kujadili kwa kina rasimu hiyo ya Katiba Mpya.

Dar es Salaam. Mwanzoni mwa wiki hii Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilizindua rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekeza kuwapo kwa mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa utawala nchini, huku yakionekana kuwa machungu kwa chama tawala cha CCM.

Tayari CCM kimetangaza kufanya mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho ili kuichambua na kujadili kwa kina rasimu hiyo ya Katiba Mpya.

Jana vyombo vya habari vilimnukuu Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana katika mkutano wake na waandishi wa habari akisema kuwa wataichambua na kuijadili rasimu hiyo.

Pamoja na mambo mengine, rasimu hiyo ya Katiba Mpya imependekeza kuwapo kwa Serikali tatu; Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi na kufutwa kwa viti maalumu vya ubunge.

Mapendekeo hayo yametolewa ikiwa ni miezi sita tangu vyama mbalimbali vya siasa kuwasilisha maoni yao kwa tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kupendekeza mambo mbalimbali ikiwamo muundo wa Serikali, Uchaguzi Mkuu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mapendekezo ya CCM

Katika mapendekezo yake CCM walitaka ubaki mfumo wa Serikali mbili kama ilivyo sasa, ikieleza kuwa hauna gharama, huku kikieleza kwamba uzoefu katika nchi nyingi za Afrika unathibitisha kushindwa kwa mfumo wa Serikali tatu na ule wa Serikali ya Shirikisho (Federation government).

Hata hivyo, mapendekezo ya rasimu hiyo yanaonyesha kuwa Jamhuri ya Muungano itakuwa na muundo wa shirikisho lenye Serikali tatu na kwamba shughuli zote za muungano zitasimamiwa na Serikali, Bunge na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano, hivyo kukifanya CCM kuanguka katika maoni kuhusu suala hilo.

CCM ilipendekeza sera ya dola kutokuwa na dini rasmi, bali iruhusu kila mtu kuwa na uhuru wa kufuata dini anayoitaka mwenyewe, jambo ambalo limebaki kama lilivyo katika mapendekezo ya rasimu hiyo.

Chama hicho kimeonekana kukwama pia katika mapendekezo yake ya kuupigia debe mfumo wa sasa wa rais kushinda kwa wingi wa kura (simple majority) kwa maelezo kuwa hauna gharama pamoja na kutaka wananchi wawe na haki ya kuhoji uchaguzi wa rais.

Lakini, mapendekezo katika rasimu hiyo yanaeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano atatangazwa baada ya kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote na endapo hakutakuwa na mshindi, walioshika nafasi ya kwanza na ya pili watarudia uchaguzi ndani ya siku 60.

CCM kilipendekeza mawaziri wasitoke nje ya Bunge, huku kikitaka kuongezwa kwa wigo wa viongozi wanaoteuliwa na rais na kupitishwa na Bunge kama ilivyo kwa waziri mkuu.

Mapendekezo mengine ya chama hicho ambayo hayakupitishwa ni kuanzishwa kwa utaratibu utakaoshirikisha Bunge katika uteuzi wa baadhi ya vyombo vya utendaji ikiwemo tume ya uchaguzi na kutokuwepo mgombea binafsi .

Mbali na hayo, chama hicho pia kilitaka uwepo ukomo wa idadi ya wabunge ili kuzuia uwezekano wa kuongeza majimbo bila kuzingatia vigezo mahsusi na uwezo wa taifa.

Kuhusu wabunge wa viti maalumu CCM ilitaka idadi ya wabunge hao itokane na asilimia ya idadi ya viti iliyopata chama baada ya kushinda uchaguzi.

Kuhusu kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa rais, CCM ilitaka uwepo utaratibu maalumu wa kupinga matokeo hayo na siyo mahakamani.

Chadema

Kwa upande wa Chadema kilipendekeza kuanzishwa kwa utawala wa majimbo yasiyozidi kumi ili kuleta uwiano katika matumizi ya rasilimali kwenye maeneo yote ya nchi. Hata hivyo, rasimu hiyo ilipendekeza kutokuwepo kwa Serikali za majimbo ikieleza kungechochea mgawanyiko ambao ungejengwa kwa misingi ya udini, ukabila na ukanda.

Chadema pia kilipendekeza umri wa kugombea ubunge ushushwe hadi miaka 18 ili kutoa nafasi kwa mtu yoyote kuwa na haki ya kupiga au kupigiwa kura, lakini rasimu hiyo imeeleza kuwa umri wa mtu kugombea ubunge ni miaka 21 huku ikitaja umri wa kugombea urais kuwa ni kuanzia miaka 40.

Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chama hicho kilipendekeza iwe na wajumbe 25 kati yao 15 watokane na vyama vyenye uwakilishi bungeni na wateuliwa kwa uwiano wa wabunge walioko bungeni, wengine watoke kwenye asasi za kiraia, vyama vya wakulima, jumuiya za kidini na vyama vingine vya siasa visivyo na uwakilishi bungeni na mwenyekiti na makamu wake wateuliwe na wajumbe wenyewe.

Katika hilo chama hicho kimekwama kwani rasimu imependekeza kuwa wajumbe wa tume hiyo watateuliwa na rais.

Mapendekezo ya chama hicho ambayo yamepitishwa na tume ni pamoja na kuwepo kwa Serikali tatu, matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani.

CUF

Ilipendekeza kuwapo Katiba tatu zitakazoongoza Serikali za Tanganyika, Zanzibar na Muungano jambo ambalo limependekezwa pia na Rasimu ya Katiba Mpya.

Chama hicho pia kilipendekeza mgombea binafsi katika nafasi ya urais, kupunguzwa kwa madaraka ya rais na rais apatikane kwa kupata zaidi ya asilimia 50.