Ray C 'Unene ulinitesa kama dawa za kulevya'

Ray C

Mmoja wasanii wa kike Bongo aliyewahi kupitia misukosuko hadi serikali kuingilia kati ni Rehema Chalamila maarufu kwa jina la Ray C.

Kwa wale mnaokumbuka kipindi ambacho Bongo Fleva inaanza kuwika, Ray C alikuwa kati ya wanamuziki wa kike aliyefanya vizuri, huku akitamba na nyimbo kadha wa kadha ikiwemo Uko Wapi, Upepo, Mahaba ya Dhati, Sogea Sogea na Umenikataa.

Pamoja na misukosuko ya matumizi ya dawa za kulevya, unene ni moja kati ya kadhia iliyokuwa ikimkabili.

Akizungumza na Mwananchi, Ray C anafichua moja ya sababu ya kupungua na kurudi katika hali yake ya zamani kuwa imetokana asili ya familia yao kutokuwa na watu wanene.

“Unajua kwetu wengi asili yetu ni wembamba hivyo ilikuwa rahisi mimi pamoja na kufanya mazoezi kupungua kwa haraka, kwani kupungua nako ni kazi kama hutafuata masharti na pia ukiwa na asili ya unene,” anasema Ray C.

Aeleza kero alizokuwa akipata kutokana na Unene

Moja ya matatizo ambayo Ray C anaeleza kuwa alikuwa akipata alipokuwa mnene ni pamoja na shinikizo la damu.

Kitendo hicho anasema kilikuwa kikimfanya aheme kwa tabu ambapo daktari wake alimwambia ni lazima kutafuta suluhu ya kupungua.

“Maana haipiti wiki lazima presha ipande mpaka manesi walikuwa wananishangaa na walivyonitisha kuwa naweza kufa nikiendelea na unene ule ikabidi nitafute suluhisho la kufanya mazoezi na kupunguza kula na kufanya kila aina ya diet,” anabainisha Ray C.

Hata hivyo, anakiri kwamba kupungua sio kazi rahisi, japo aliamua kujituma kufanya hivyo kwa kuwa yeye kawaida yake si mtu wa kukata tamaa kirahisi

“Naomba niwashauri wale vibonge kuwa wembamba ndo dili unene uchafu tu kwani hata kujisugua bafuni vizuri tabu ukipindisha tu mkono mgongoni unahema kama umefanya jogging kumbe unaoga tu, yaani binafsi sitaki kuusikia kabisa,” anasema.

Anaongeleaje mipango yake

kwenye muziki

Ray C anasema katika kurudi kwenye soko la muziki rasmi tayari ameshaanza kutengeneza albamu yake huku kazi zake nyingi akizifanyia nchini Nairobi.

Anasema albamu hiyo anatarajia kuiachia kuanzia Juni mwaka huu, na kuwataka mashabiki wake kukaa mkao wa kule kwa kuwa Ray C waliokuwa wanamfahamu ni yuleyule.

“Yaani kila nikiangalia nyimbo nilizowahi toa mpaka leo basi najiuliza niliwezaje kuandika nyimbo nzuri kiasi kile hadi leo zinapendwa na bado huwezi shindanisha na nyimbo za sasa.

“Maana za sasa hazidumu na asikuambie mtu katika wasanii najikubali kuweka alama yangu ya milele kwenye hii sanaa yetu hata nikifa leo vizazi vijavyo vitanijua nilikuwa nani hapa Tanzania,” anasema Ray C.

Nani anamsimamia kwa sasa?

Kuhusu mtu anayemsimamia, msanii huyu anasema kwa sasa yupo chini ya kampuni ya Maliza Umaskini iliyopo chini ya taasisi isiyo ya kiserikali.

Alipotakiwa kueleza sababu ya kukaa Nairobi anasema: “Pia riziki popote na kusafiri ndio kupata fursa na watu mbalimbali na kujikuza kiakili pia! kuzubaa sehemu moja hasa kwa sisi wasanii lazima utaumia hasa sanaa yetu hii ya Bongo ambayo umaarufu ni zaidi kuliko mfuko kwa hiyo lazima uchangamshe akili,” anasema.

Ray C Foundation imeishia wapi?

Baada ya kunusurika katika utumiaji wa dawa za kulevya, msanii huyu alianzisha taasisi yake aliyoipa jina la Ray C Foundation, lengo likiwa ni kupambana na matumizi ya dawa hizo hususani kwa vijana waliokuwa wameathirika na tatizo hilo.

Hata hivyo anasema kwa bahati mbaya kampeni yake hiyo ilikuwa inapingwa na wahusika wenyewe na kumsababisha asipate msaada ambapo anakiri kitendo hicho kilimuumiza.

“Hii kitu ya kupigwa vita kwa kweli iliniumiza sana ukizingatia nilikuwa na lengo zuri kwa vijana wa Kitanzania kwa kuwa mimi nilipitia huko najua madhara yake.

“Laiti waliokuwa wanapambana na mimi wangejua vijana na watoto wao walivyoharibika naamini wangekuwa mstari wa mbele kusapoti hili kwa kuwa naamini baada ya miaka kumi ijayo hali itakuwa mbaya sana, tunawaona kuanzia wasanii, watu wa kawaida mpaka wenye nyadhifa za juu nao wameathirika na hili tatizo, anaeleza.

“Ndio hii sasa maana halisi ya Ray C Foundation ambayo ni matumaini, ujasiri na uthubutu wa kukabiliana na changamoto yoyote ile maishani,” anabainisha.