Ridhiwani amwagiza Mwijage kwa JPM

JIWE LA MSINGI: Waziri wa viwanda, Biashara na Uwekezaji,  Charles Mwijage (wa nne kutoka kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo (wa tatu kutoka kushoto), mkurugenzi mkuu wa kiwanda cha kutengeneza vigae cha Twyford Ceramics, Jack Feng (wa pili kutoka kulia) na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kulia) wakiweka udongo kwenye jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho eneo la Pingo, Chalinze mkoani Pwani jana. Picha na Julieth Ngarabali

Muktasari:

NUKUU

“Nakerwa sana, maana wakati mwingine wananchi wanapiga simu wanahoji, nafsi yangu inaumia sana kwa sababu jimbo hili nilipogombea sikuja kutafuta cheo bali kuwasaidia wana Chalinze.”

Ridhiwani

Pwani. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amemuomba Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage amfikishie  Rais John Pombe Magufuli (JPM) salamu za wananchi  wa jimbo hilo kuwa wanahitaji maji.

Ridhiwani alitoa ombi hilo jana Ijumaa katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Vigae cha Twyford kinachojengwa na raia wa China katika Kijiji cha Pingo wilayani hapa.

Mbunge huyo alisema kiwanda hakiwezi kuwa bora bila watu lakini wana shida kubwa ya maji.

“Chalinze ni eneo zuri kwa kiwanda cha aina yoyote, bado kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji, Serikali ya Tanu iliahidi kulimaliza na baadaye CCM, mwaka 2003 tulishuhudia mradi mkubwa wa maji wa Wami Chalinze ukizinduliwa chini ya ufadhili wa China, lakini hadi leo hatuna maji,” alisema.

Alisema baada ya kuona mradi huo unasuasua alifanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho  kuona namna ya kutumia chanzo kingine cha maji cha Mto Ruvu ili wanapovuta kupeleka huko watoe fursa kwa wananchi kuyapata.

Akizungumza kiwandani hapo, Waziri Mwijage aliwataka wananchi katika mpango wa upitishaji mradi huo wa maji kutoka Mto Ruvu wasiweke kikwazo cha kutoa eneo la ardhi ya kupitisha maji kwa kudai fidia.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema halmashauri zote zinaendelea kutenga maeneo ya viwanda kwa wawekezaji.

Aliwataka wawekezaji wa kiwanda hicho na vingine kuzingatia matakwa ya maeneo wanayowekeza mali zao kwani wakazi wa eneo husika ndiyo walinzi wakuu.

Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho, Jack Feng alisema kampuni hiyo itawekeza Dola milioni 56 za Marekani (Sh120 bilioni) katika ujenzi wa kiwanda, ununuzi wa mitambo na vifaa mbalimbali.

Alisema kampuni hiyo itakapokamilika itatoa ajira zaidi ya 6,000 kwa Watanzania zikiwamo 2,000 za kudumu.

Pia, alisema  zaidi ya asilimia 95 ya malighafi zitakazotumika kwa ajili ya kutengeneza vigae hivyo zitatoka Tanzania.