Ripoti uchunguzi kifo cha Akwilina yazua tafrani Muhimbili

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa (katikati) akizungumza na ndugu wa marehemu Akwilina Akwiline katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam jana kabla ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa kifo cha marehemu huyo. Picha na Salim Shao.

Muktasari:

  • Jambo hilo lilizua sintofahamu kabla ya kutulizwa kwa kuelezwa kwa mdomo na madaktari kuwa alipigwa risasi kichwani.

Dar/Moshi. Ndugu wa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi, jana walisusia kwa muda kuchukua mwili wa binti huyo wakishinikiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kueleza sababu za kifo chake.

Jambo hilo lilizua sintofahamu kabla ya kutulizwa kwa kuelezwa kwa mdomo na madaktari kuwa alipigwa risasi kichwani.

Jana asubuhi, ndugu hao walikusanyika katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili wakisubiri uchunguzi ukamilike ili kujua hatima ya kuusafirisha mwili kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro Ijumaa baada ya mwili huo kuagwa Alhamisi katika viwanja vya NIT, Mabibo.

Wakati wakiendelea kuvuta subira walielezwa na madaktari waliochunguza mwili huo kuwa ripoti ya uchunguzi itatolewa baada ya siku 14 jambo ambalo hawakukubaliana nalo, huku dada wa mwanafunzi huo, Tegolena Uiso akisema hawatapokea mwili bila kuelezwa nini kilichomuua ndugu yao.

“Sisi tumekuja kwa ajili ya kujua hasa ndugu yetu nini kimemkuta hatuwezi kupokea mwili bila ripoti. Wanatuambia ni baada ya wiki mbili sina hakika kama hawajabaini kitu chochote, hatuwezi kuuchukua mwili mpaka tupewe sababu,” alisema Tegolena.

Tegolena alisema walizungumza na Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zakaria Mganilwa aliyekuwa akiwasiliana na madaktari hao, mpaka saa saba mchana hawakuwa na majibu yoyote.

Awali, Profesa Mganilwa alisema wamefika hospitalini hapo kufuatilia uchunguzi huo akiwa na ndugu wa marehemu.

Akwilina alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi wa Ugavi katika chuo hicho.

Alipigwa risasi Februari 16 eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliokuwa wakielekea katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai hati ya viapo vya mawakala.

Mwili wake ulihifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kabla ya kuhamishiwa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ambao ndugu hao walifika jana hospitali hapo ili kujua sababu ya kifo chake.

Mwananchi lilishuhudia ndugu wa Akwilina wakiwa wamesimama kwa vikundi nje ya chumba hicho cha kuhifadhia maiti, na ilipofika saa nane mchana, Profesa Mganilwa alionekana kuzungumza na madaktari na baadaye kuwaeleza ndugu hao majibu ya uchunguzi.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu walichoelezwa, shemeji wa mwanafunzi huyo, Festo Kavishe alisema uchunguzi umeonyesha Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.

“Ripoti ambayo tumepewa imeonyesha kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa vibaya na risasi ambayo iliingilia upande wa kushoto kwa kichwa chake na kutokea upande wa kulia ambao umefumuka vibaya,” alisema.

Alisema wameridhishwa na sehemu ya ripoti ya uchunguzi huo na sasa wanakwenda kufanya kikao cha ndugu kujadili namna gani watampumzisha Akwilina.

Alisema iwapo madaktari wasingewapatia majibu hayo, wasingethubutu kuuchukua mwili huo kwa mazishi, kwa sababu walihitaji kupata picha kamili ya nini kilimuua Akwilina.

“Sasa tumeshafahamu nini kimemuua ndugu yetu kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na madaktari baada ya uchunguzi, hivi sasa tunakwenda kujadiliana kuhusu mazishi yake,” alisema Kavishe jana.

Mazishi ya Akwilina

Baada ya kutoka Muhimbili, ndugu hao walifanya kikao cha kupanga shughuli ya mazishi na baadaye kaka wa marehemu, Moi Kiyeyeu kueleza kuwa Akwilina atazikwa Ijumaa. “Tutamuaga ndugu yetu siku ya Alhamisi katika viwanja vya chuo cha NIT pale Mabibo na siku hiyohiyo tutaanza safari kuelekea Rombo-Mashati Olele mkoani Kilimanjaro na mazishi tutafanya Ijumaa,” alisema Kiyeyeu.

Baba atamani kumkabili muuaji

Akwiline Shirima, ambaye ni baba mzazi wa Akwilina katika mahojiano na Mwananchi jana alisema siku akikutana na polisi aliyemuua mwanae, atapambana naye.

Wakati baba akiapa kupambana na muuaji wa mwanae kama atakutana naye, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliomba kuundwa tume huru kuchunguza mauaji hayo.

Akizungumza nyumbani kwake Kijiji cha Olele jana, Shirima alisema endapo muuaji atakuwa ni kijana mwenye nguvu kumzidi, atapambana naye hata kwa kumuuma kwa meno.

“Najua ni ngumu kukutana na aliyempiga mwanangu risasi, lakini laiti ningekutana naye kama ni kijana mwenye nguvu kunizidi ningepambana naye hata kumuuma kwa meno,” alisema.

“Na kama ni mzee mwenzangu ningepambana naye hadi kifo ila kwa bahati mbaya siwezi kumpata hivyo sina namna. Kwa kweli hiki kifo kimezima ndoto ya familia ya kuondokana na umaskini.”

Shirima aliiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwa kina na kuona namna ya kumsaidia kwa kuwa tegemeo lake limeondoka na wao kwa sasa hawana msaada wowote na wanachosubiria ni kifo.

“Jamani hii ni taa yangu imezimika na kuniacha gizani kwani tangu nimepata taarifa za kifo chake sijaweza kula chochote. Nimekuwa kama nguruwe aliyetelekezwa porini bila msaada,” alisema Shirima.

“Nilipopata taarifa za kifo cha mwanangu nilishtuka sana, na kuhoji ni mwizi au nini kimetokea, lakini baadaye nikaambiwa ni polisi imefanya mambo hayo. Imenitia uchungu sana na siwezi hata kula.”

Shirima alisema afadhali mwanaye angekuwa mgonjwa akamuuguza kuliko kifo cha ghafla alichokipata ambacho kimewaacha kwenye hali ambayo haitafutika mioyoni mwao katika maisha yao yote.

Mama wa marehemu, Costanzia Akwiline alisema mauaji ya mwanaye ni ya kinyama na bora angekuwa mbuzi angekula nyama kujifariji kuliko kwa mwanaye ambaye hakuna anayeweza kumfuta machozi.

“Mwanangu hakuwa mwanasiasa, aliuawa akiwa kwenye gari akielekea kwenye shughuli zake, familia tulijinyima tukajichanga kwa kushirikiana na majirani ili asome aje atokomboe,” alisema.

“Lakini leo nasubiria niletewe maiti kwenye jeneza. Kwa kweli imeniuma sana na kunikatisha tamaa. Naomba Serikali itende haki katika tukio hili.”

Romana Akwiline, ambaye ni dada wa marehemu aliiomba Serikali kusaidia jambo hilo na kuhakikisha waliohusika na mauaji hayo aliyosema ni ya kinyama wanachukuliwa hatua ili liwe fundisho.

Akizungumzia maisha ya Akwilina, alisema baada ya mdogo wao kuonekana anapenda elimu, ndugu walijichanga kwa kushirikiana na majirani ili kuhakikisha anatimiza ndoto zake.

“Familia yetu kama mnavyoiona ni watu maskini. Wazazi wetu ni wakulima na sisi ndugu zake tumeishia darasa la saba, huyu tulidhani ndiye atakuja kuwa mkombozi wa familia,” alisema.

Alisema pamoja na matumaini hayo makubwa ya familia, hawakujua kuwa yalikuwa ni mawazo yao tu ambayo yasingeweza kutimia kutokana na mtu mmoja kuchukua uhai wake.

Alisema katika familia yao wako wanane na mtoto mwingine ambaye anasoma yupo kidato cha tatu na kwamba kutokana na tukio hilo wanaweza kukata tamaa ya kumsomesha.

“Tulitegemea marehemu anaweza kuja kumsaidia mdogo wake huko mbeleni ili naye afike chuo kikuu na kushirikiana kuikomboa familia. Hili linaweza kuwavunja moyo wanaojitolea,” alisema.

Mwanaukoo Dismas Shirima alisema marehemu alikuwa na uchungu wa maisha licha ya umri wake kuwa mdogo, hali iliyomsukuma kujituma kusoma kwa bidii ili kuinua familia yake.

“Kutokana na upeo wake na mtazamo wa kuona mbali, alijituma katika kusoma na hii iliwafanya watu wengi kutoa misaada ili apate elimu kumwezesha kutimiza ndoto zake,” alisema.

Shirima alisema ni vyema jamii ikatambua kuwa hakuna aliyepanga Akwilina auawe na waepuke kuingiza siasa katika jambo hilo.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kiwelu alisema kifo cha Akwilina kimeleta masikitiko katika jamii, hasa familia yake ambayo iliweka matarajio makubwa kwake.

Polisi watoa neno uchunguzi

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa kuhusu uchunguzi wa tukio hilo alisema polisi haiwezi kutoa taarifa wakati uchunguzi unaendelea.

“Uchunguzi unapofanyika hatuwezi kuwajulisha tukimaliza tutaeleza nani amekamatwa kwa hiyo tupeni nafasi tufanye kazi,” alisema.

Imeandikwa na Herieth Makwetta, Elizabeth Edward na Mwafatma Hamis (Dar), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi).