Ripoti yataja mambo manne kikwazo cha uwekezaji

Mkurugenzi wa Sera za Uchumi na Biashara wa Uholanzi, Eugene Gies 

Muktasari:

  • Kwenye ripoti ya mazingira ya uwekezaji ya Global Competitiveness 2017/18, iliyotolewa na Jukwaa la Kimataifa la Uchumi (WEF) kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti ya Repoa, inaonyesha kuwa utulivu wa sera za uwekezaji ndio ulioiwezesha Tanzania kupanda kwenye viwango vya kimataifa.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikifanya vizuri katika kukabiliana na rushwa kwa kuvutia wawekezaji, imeshauriwa kurekebisha maeneo manne muhimu ili kujiweka vizuri zaidi.

Kwenye ripoti ya mazingira ya uwekezaji ya Global Competitiveness 2017/18, iliyotolewa na Jukwaa la Kimataifa la Uchumi (WEF) kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti ya Repoa, inaonyesha kuwa utulivu wa sera za uwekezaji ndio ulioiwezesha Tanzania kupanda kwenye viwango vya kimataifa.

Utafiti huo uliozingatia vigezo 12 vya uwekezaji na urahisi wa kufanya biashara ulihusisha mataifa 137 na Tanzania kushika namba 113, ikiwa imepanda kwa nafasi tatu kutoka 116 iliyokuwamo mwaka 2016/17. Pamoja na mafanikio hayo, ipo nyuma ya Rwanda iliyopo namba 58 na Kenya 91.

Akiwasilisha matokeo hayo, Mkurugenzi wa Utafiti wa Repoa, Dk Lucas Katera alisema Tanzania imefanya vizuri baada ya kukabiliana vyema na vitendo vya rushwa ikilinganishwa na mataifa mengine ya EAC isipokuwa Rwanda.

Licha ya rushwa, Tanzania imefanya vizuri kuimarisha mazingira ya kisiasa kwa kutokuwa na machafuko au vurugu za namna yoyote zinazoweza kuwatisha wawekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya afya.

Wakati mpango wa bima kwa wote unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukilipaisha taifa, sera nzuri za ajira nazo zimetajwa kuwa rafiki hasa kwa kuruhusu wataalamu kupata vibali vya kazi bila usumbufu. Hilo ni sambamba na matumizi ya fedha za kigeni.

Hata hivyo, watafiti hao wanashauri kufanywa marekebisho kwenye baadhi ya maeneo ili kuwashawishi zaidi wawekezaji hasa wa kimataifa. Maeneo manne yametajwa hapa ambayo ni uboreshaji wa miundombinu, kodi, upatikanaji wa mikopo na ubunifu katika elimu.

Katera alisema licha ya juhudi za Serikali kujenga barabara na reli ya kisasa (SGR), gharama za usafiri wa anga zipo juu na umeme si wa uhakika na kwamba, wawekezaji wengi waliohusishwa walilalamikia viwango vikubwa vya kodi.

Kuhusu taasisi za fedha nazo, wawekezaji walisema wakati wao wakitaka mikopo mikubwa itakayolipwa kwa riba ndogo, benki zinataka faida ya haraka. Pia, taasisi za elimu ya juu zimetupiwa lawama kwa kutofundisha ujuzi unaohitajika sokoni hivyo kuwafanya wahitimu washindwe kushindana ndani hata kimataifa.

Naye Mkurugenzi wa Sera za Uchumi na Biashara wa Uholanzi, Eugene Gies alisema ingawa ni vigumu kuilinganisha na Tanzania, elimu ya nchini kwake inaruhusu ubunifu na sera huwa hazibadiliki mara kwa mara.

“Viwango vya kodi ni vikubwa kuliko Tanzania lakini watu wanafurahia kulipa,” alisema.

Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Ammon Mbelle alisema iwapo uwekezaji utaendelea kufanywa kwenye miundombinu, Tanzania itafanikiwa kutimiza ndoto yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.