Monday, June 19, 2017

Ripoti za makinikia zachagiza 400 kuvamia mgodi wa Acacia

 

By Waitara Meng’anyi na Dinna Maningo, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Zaidi ya vijana 400 kutoka kata za Kemambo Matongo Wilaya ya Tarime, wamevamia mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia wakishinikiza fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa na kampuni hiyo kupisha uchimbaji wa dhahabu.

Hatua hiyo inahusishwa na ripoti ya pili ya kamati maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini katika makontena 277.

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ilibaini kuwa kampuni ya Acacia haitambuliki kwa kuwa haijasajiliwa rasmi nchini.

Akizungumza kwa simu jana, mkazi wa Kijiji cha Matongo, Adamu Kibe alisema vijana hao walichukua hatua hiyo baada ya kuingiwa hofu ya Acacia kuondoka au kufukuzwa bila wananchi kulipwa fidia kwa kuwa haijasajiliwa.

“Kinachotutia hofu ni taarifa za kamati za uchunguzi za Rais Magufuli, hasa ile iliyobaini kuwa kampuni hii haiko nchini kihalali kwa sababu haijasajiliwa Brela,” alisema Kibe.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya lilizima jaribio hilo kwa kuwatanya vijana hao kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya, Andrew Satta alisema hakuna mtu aliyeshikiliwa wala kujeruhiwa wakati wa tukio hilo lililotokea jana na kudumu kwa zaidi ya saa moja.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Emmanuel Ngocho alisema vijana hao walitoka katika vijiji vitatu vya Kewanja, Nyangoto na Matongo.

“Pamoja na ukweli kwamba vijana hawa ni wale wanaotafuta mchanga wa dhahabu ili kujipatia kipato kutokana na hali yao ya kiuchumi kuyumba, walijificha nyuma ya madai ya fidia ili kuhalalisha tukio hilo,” alisema Ngocho.

Mkazi wa Nyangoto, Dominic Nyamohanga aliunga mkono kauli ya hali ngumu kimaisha kuwa chanzo cha uvamizi wa vijana hao ambao lengo lao kuu lilikuwa kupata mchanga wa dhahabu baada ya mgodi kusitisha kumwaga mabaki ya mchanga kwa wananchi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Madai ya fidia

Tangu mwaka 2014, baadhi ya wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo wamekuwa wakisubiri malipo ya fidia baada ya maeneo yao kuingizwa ndani ya eneo la mwekezaji au kuhamishwa kupisha madhara yatokanayo na shughuli za uchimbaji ikiwamo mitikisiko inayosababishwa na milipuko ya baruti pamoja na vumbi.

Baadhi yao tayari wamelipwa huku wengine malipo yao yakichelewa kutokana mvutano ulioibuka kuhusu tathmini na kiasi cha fedha ikilinganishwa na thamani halisi ya ardhi na mali.

Akizungumzia vurugu hizo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Rashid Bogomba aliwataka wakazi wa Nyamongo kuwa watulivu na kuepuka matumizi ya nguvu kudai haki zao.

“Kila mtu, hasa sisi viongozi na wawakilishi wa wananchi tunapenda suala hili la fidia lifikie mwisho kwa kila anayestahili kulipwa, lakini matumizi ya nguvu ikiwamo kuvamia eneo la mwekezaji siyo njia ya sahihi ya kudai malipo,” alisema Bogomba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kemambo-Nyamongo.

Tangu mwaka 2010 baadhi ya wananchi walipofanyiwa tathmini ya ardhi na mali zao, wahusika wamezuiwa kuendeleza au kufanya shughuli yoyote ya kimaendeleo kusubiri fidia.

Mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliunda kamati iliyoshirikisha wawakilishi wa wananchi, mwekezaji, viongozi wa maeneo yanayopakana na mgodi pamoja na wataalamu kuchunguza kiini cha mvutano huo.

Akichangia hotuba ya bajeti kwa mwaka 2017/18 bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita, Mbunge Tarime Vijijini, John Heche alionya kuwa uvumilivu wa wakazi wa Nyamongo kuhusu madhila wanayopata kutokana uwekezaji wa mgodi wa dhahabu umefika mwisho.

-->