Saturday, August 12, 2017

Roma Mkatoliki avunja ukimya kwa mafumbo

 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi mjumanne@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi minne tangu kuripotiwa kutekwa kwa msanii Ibrahim Mussa maarufu kama Roma jana ametoa wimbo wake ambao umepokewa kwa mitazamo tofauti.

Katika wimbo huo ambao ulitoka juzi ukiitwa ‘Zimbabwe’, ametumia lugha ya kufikirisha na video ambayo imetumia picha zilizo na ujumbe mbalimbali.

Wakati akitambulisha wimbo huo, Nancy Mshana ambaye ni mume wa msanii huyo alisema amesafiri kwenda Zimbabwe hivyo kushindwa kuutambulisha rasmi wimbo huo.

Wimbo huo una maeneo ambayo yamezua maswali miongoni mwa mashabiki hapa pale alipozungumzia tukio la kutekwa kwake.

“Walioniteka hawakuja na Noah, ni uvumi na visange,” ni moja kati ya mashairi ya wimbo huo ambayo katika taarifa za kutekwa kwake ilielezwa kuwa alichukuliwa na gari la aina hiyo.

Pia Roma ametumia wimbo huo kuacha maswali ambayo yameilenga familia yake pindi akitolewa uhai. Julai 8, Roma alizungumza na waandishi wa habari na kuelezea jinsi alivyotekwa na akiwa na wenzake watatu na usalama wao ulivyo kuwa shakani huku akiwataka mashabiki kutohusisha tukio hilo na kutafuta umaarufu.

Pamoja na kutoa wimbo uliojaa mafumbo, mwanamuziki huyo amewaachia maswali mashabiki wake juu ya maana halisi ya wimbo huo na sababu za kuuita Zimbabwe na iwapo ni kweli amesafiri kuelekea huko.

-->