VIDEO: Ronaldo apokewa kishujaa Juventus

Muktasari:

Nguli huyo alitarajiwa kutia saini mkataba wa miaka minne na atavuna Euro 30 milioni kwa msimu mmoja.

Turini, italia. Maelfu ya mashabiki wa Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin, wamejitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Allianz mjini Turin, kumpokea mshambuliaji wao mpya, Cristiano Ronaldo.

Ronaldo aliwasili jana mjini Turin kwa ndege binafsi ya kukodi na kwenda moja kwa moja Hospitali ya J Medical Centre, kufanyiwa uchunguzi wa afya huku maelfu ya mashabiki wakisubiri kwa hamu utambulisho wake.

Mashabiki walijipanga kando ya barabara jirani uwanja huo wakiimba “Ronaldo, Ronaldo, tupe nasisi ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya”.

Hata hivyo, mshindi huyo mara tano wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia ‘Ballon d’Or’, alitia saini vitabu vya baadhi ya mashabiki wakiwemo watoto waliokuwa wamevaa jezi za Juventus.

Nguli huyo alitarajiwa kutia saini mkataba wa miaka minne na atavuna Euro 30 milioni kwa msimu mmoja.

Uhamisho wake kutoka Real Madrid umeigahrimu Juventus Euro 100 milioni lakini baadhi ya vyombo vya habari vinadai kuwa uhamisho huo umechukuwa zaidi ya Euro 350 milioni.