Rufaa yamtoa gerezani diwani wa Chadema

Muktasari:

Kuachiwa kwa diwani huyo juzi jioni na Mahakama hiyo kulitokana na rufaa aliyokata kupinga adhabu hiyo aliyopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya.

Mbeya. Ikiwa ni takriban mwaka mmoja na mwezi mmoja tangu alipohukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani, Diwani wa Kata ya Iganjo jijini hapa kupitia Chadema, David Mwangonela ameachiwa huru na Mahakama Kuu.

Kuachiwa kwa diwani huyo juzi jioni na Mahakama hiyo kulitokana na rufaa aliyokata kupinga adhabu hiyo aliyopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya.

Mwangonela alihukumiwa kutumikiwa adhabu hiyo baada ya kukutwa na magunia 171 ya ngano yaliyodaiwa kuibwa kwenye Chuo cha Utafiti na Kilimo Uyole.

Kabla ya adhabu hiyo wakati kesi ikisikilizwa watu wanne walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi na kusomewa mashtaka manne.

Mashtaka hayo yalikuwa ni kuvunja ghala, wizi wa magunia 171 ya ngano, kupatikana na mali ya wizi na kuzembea kuzuia kosa.

Washtakiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Ibrahim Mwangu, Juma Mwatumeli, Andrea Nsoka na David Mwangonela, lakini Mahakama ilimkuta na hatia mshtakiwa wa wanne, Mwangonela hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela ambacho alianza kukitumikia Novemba 17, 2015 huku wengine wakiachiwa huru.

Hata hivyo, Mwangonela alikata rufaa kupinga hukumu hiyo katika Mahakama Kuu jijini hapa ambayo ilianza kusikilizwa Aprili mwaka huu chini ya Jaji Mfawidhi, Noel Chocha.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Chocha alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi ilimshtaki Mwangonela kwa kutumia vifungu vya sheria ambavyo vilikosewa, hivyo viini vya shtaka pia vilikuwa na makosa.

Alisema kutokana na kukosewa kwa viini vya shtaka alilokutwa nalo mshtakiwa huyo, Mahakama hiyo inaona hana hatia na kumuachia huru.

Pia, Mahakama iliagiza arudishiwe magunia 171 ya ngano au kiasi cha fedha kinacholingana na thamani yake.

“Mahakama inaamuru David arudishiwe magunia yake 171 ya ngano ambayo yalikuwa yamezuiwa au apewe fedha zinazoendana na thamani ya magunia hayo na yupo huru kuanzia sasa,” alisema Jaji Chocha.

Akizungumza na gazeti hili nje ya Mahakama, Mwangonela alisema Mahakama Kuu imemtendea haki ambayo aliporwa na kuwashukuru wapiga kura wake kwa uvumilivu waliouonyesha tangu akumbwe na mkasa huo, hivyo kushindwa kuwatumikia tangu walipomchagua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.