Ruge atoboa siri ya ujasiriamali wenye tija

Muktasari:

Ruge alitoa rai hiyo jana katika kongamano la kujadili masuala ya ujasirimali, lililoandaliwa na Kituo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDIEC).

Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amewataka vijana nchini wasisubiri kushindwa maisha kwingine ndiyo waanze kuingia kwenye ujasiriamali.

Ruge alitoa rai hiyo jana katika kongamano la kujadili masuala ya ujasirimali, lililoandaliwa na Kituo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDIEC).

“Nadhani ifike mahali ujasirimali uanzie ndani ya familia zetu na si tuanze baada ya kufeli maisha, hiyo haitasaidia kwa kuwa ni jambo ambalo hautakuwa unalifanya kutoka ndani ya moyo wako,” alisema mkurugenzi huyo.

Ruge alisema kwamba wakati vijana wengi wakilalamikia suala la mitalaa ya shule kuwa sababu ya kutojiajiri, kwake hilo halina maana kwa kuwa ujasiriamali unaanzia ndani ya moyo.

Alisema ni lazima watu wabadili akili zao kwa kupenda kufanya jambo bila ya kusukumwa au kwa kuwa tu ameshindwa sehemu fulani.

“Haiwezekani kijana una umri mdogo na nguvu ya kufanya kazi unalala saa 12 au unasubiri uambiwe ufanye kitu bila ya wewe kujituma na kuwa mbunifu, ndiyo maana hata Serikali imetoka kwenye mfumo wa ujamaa na kuukubali ubepari ili kila mtu awe huru kufanya jambo lake na hapa ndiyo inapotokea mtu aliyepata kapata na aliyekosa kakosa hivyo hamna namna kila mmoja wetu ajitume ipasavyo,”alisema Ruge.

Awali, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu), Stella Ikupa alisema Serikali itaendelea kuwajengea vijana mazingira mazuri ya ufanyaji biashara.

Ikupa alisema wataendelea kuwawezesha vijana kuendeleza mawazo ya ujasiriamali ikiwamo kuwadhamini masomo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uvumbuzi na Ujasiriamli kutoka UDEIC, Abraham Temu alisema kwa miaka kumi sasa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, wamekuwa wakiandaa mashindano ya uandikaji michanganuo ya biashara kwa wanafunzi.