Rungwe asema hatachoka kutoa salamu za rambirambi hadi...

Muktasari:

Chama cha Chaumma kimesema Serikali inahitaji kuweka mikakati ya kuhakikisha inazuia ajali za majini kwa wahusika wa usafiri kuzingatia ubebaji wa abiri na mizigo na kutoa elimu kwa  wananchi wanaovitumia vivuko hivyo kuwa makini.

Chaumma kimesema hakitachoka kutoa salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli hadi pale Serikali itakapowajibika ipasavyo kusimamia usafiri wa majini na nchi kavu.

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma ( Chaumma), kimetoa salamu za  pole kwa Rais John Magufuli kutokana na ajali ya kivuko cha Mv Nyerere huku kikimshauri mambo manne ya kufanya ili kukabiliana na ajali kama hizo nchini.

Pia, Chaumma kupitia kwa Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe kimetoa ubani wa Sh300,000 kupitia akaunti iliyotangazwa na Serikali ya kuchangia waathirika wa Kivuko cha Mv Nyerere.

Rungwe amesema ingawa Rais Magufuli amechoka kutoa salamu za pole kwenye ajali, Chaumma kitaendelea kumpa salamu hizo kwa niaba ya Watanzania hadi pale Serikali itakapowajibika kikamilifu kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 25,218, Rungwe amesema Chaumma kimesikitishwa na ajali hiyo na kimeishauri Serikali kuweka utaratibu maalumu kwa watu wanaokatisha tiketi ili idadi kamili ya abiria wanaopanda iwe rahisi kubainika.

"Serikali iangalie watu wanaohusika idara ya mizigo  wawe makini na mizigo inayotakiwa kusafirishwa na chombo husika.”

“Pia, Serikali iweke utaratibu wa kuvikagua mara kwa mara vyombo ili kuvibaini ubora wake," amesema Rungwe.

Rungwe ambaye alikuwa mmoja wa wagombea urais  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa Oktoba 25 mwaka 2015, amesema ni wakati muafaka sehemu zinazohitaji vivuko kupewa vivuko vya kisasa kama ilivyofanya kwenye ndege.

Jambo jingine aliloshauri Rungwe ni Serikali kuhakikisha inaimarisha ulinzi wa abiria wakati wa kupanda na kushuka hasa kuwazuia wasisogelee kwenye lango kabla ya kivuko hakijatia nanga.

Kivuko cha Mv Nyerere kilizama katika Kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe Septemba 20, 2018 na kusababisha vifo vya watu 227 na manusura 41.