Rungwe naye ataka kwenda Ikulu

Muktasari:

Hashim Rungwe amesema anatamani kwenda Ikulu kuonana na Rais John Magufuli ili kumweleza mambo ambayo yatawezesha kusaidia kuleta mabadiliko katika utawala wake

Dar es Salaam. Mwenyekiti Chama cha Chaumma, Hashim Rungwe amesema anatamani kwenda Ikulu kuonana na Rais John Magufuli ili kumweleza mambo ambayo yatawezesha kusaidia kuleta mabadiliko katika utawala wake.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 12, 2018, Rungwe amesema kila mtu anatamani kuonana na Rais Magufuli lakini nafasi hiyo imekuwa haipatikani.

Rungwe anatoa kauli hiyo ikiwa imepita siku tatu tangu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alipofanya ziara Ikulu na kuzungumza na Rais Magufuli.

“Hata mimi nataka kuonana na Rais, nimekuwa natamani sana lakini hatupati nafasi hiyo, nikikutana naye tutazungumza mambo mengi, ambayo yatamsaidia yeye mwenyewe katika uongozi wake,” amesema Rungwe na kuongeza;

“Sisi upinzani tulikuwa tunasema hatutaki mafisadi, hatutaki wabidhirifu au tunapiga kelele dawa hakuna hospitalini kwa hiyo anapopeleka dawa hospitalini ni sisi tumesaidia, kwa hiyo kuongoza ni kusikiliza watu wanasema nini wakati mwingine.”

Mwananchi lilipotaka kujua hasa ni kitu gani ambacho anataka kumweleza Rais Magufuli, Rungwe amesema “hiyo ni siri yangu, lakini tumekuwa tikitafuta nafasi hiyo lakini wapi, lakini naona Lowassa kaenda na wamezungumza.”