Vitendo vya rushwa Tanga vyaongezeka

Muktasari:

Kuhusu uendeshaji wa kesi, Mariba amesema Takukuru Mkoa wa Tanga imeendesha kesi 18 mahakamani ambapo kati ya hizo 9 zilifunguliwa kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Desemba 2017 na kesi 9 ni za kabla ya Julai 2017.


Tanga.Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) imepokea taarifa 204 za vitendo vya rushwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Christopher Mariba amesema hayo leo Februari 18, 2018 wakati akitoa  taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi

cha miezi sita iliyopita.

Amesema kati ya taarifa 52 zilizohusu Serikali za mitaa, idara ya ardhi pamoja na mabaraza ya ardhi yameongoza kwa kuwa na matukio 33 yaliyoripotiwa, zikifuatiwa na vyama vya siasa vyenye taarifa 28, polisi 23, elimu 18, mahakama 16, afya 15, kilimo 8,Tasaf 5, huku

mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA),maji ,ushirika,uhamiaji,Tanesco na misitu zikiwa na taarifa moja kila  idara.

Amesema kati ya taarifa hizo 204 zilizopokewa,92 zinaendelea na kuchunguzwa ,66 uchunguzi wake umekamilika,na majalada kufungwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi huku taarifa 46 zikihamishiwa idara nyingine kutokana na kutoihusu Takukuru.

Kuhusu uendeshaji wa kesi, Mariba amesema Takukuru Mkoa wa Tanga imeendesha kesi 18 mahakamani ambapo kati ya hizo 9 zilifunguliwa kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Desemba 2017 na kesi 9 ni za kabla ya Julai 2017.