#WC2018: Russia yajipigia Saudi Arabia

Muktasari:

Russia imepata ushindi wa kwanza tangu Oktoba mwaka jana.

Moscow, Russia. Wenyeji wa Kombe la Dunia, Russia wametuma salamu kwa wapinzani wake wa Kundi A baada ya kuichakaza Saudi Arabia kwa mabao 5-0 katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Moscow.

Ushindi huo unaifanya Russia kuongoza Kundi A kwa pointi tatu na mabao matatu kabla ya mechi ya kesho kati ya Uruguay na Misri.

Wenyeji walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika 12 lililofungwa na Iury Gazinsky akitumia vizuri makosa ya mabeki wa Saudi Arabia.

Dakika 23, wenyeji Russia wamepata pigo baada ya nyota wao Alan Dzagoev kuumia na kushindwa kuendelea  mchezo huo nafasi yake kuchukuliwa na Denis Cheryshev.

Cheryshev aliwasahaulisha machungu Russia baada ya kufunga bao pili dakika 43, akiwalamba chenga mabeki wa Saudi Arabia na kupiga shuti lilojaa wavuni.

Kipindi cha Pili Saudi Arabia walionekana kubadilika, lakini washambuliaji wake walikosa umakini katika kumalizia mashambulizi yao.

Wenyeji Russia ikiwa na lengo mmoja tu la kujiweka vizuri katika kundi hilo na kujihakikishia kufuzu kwa hatua 16 bora waliendelea kucheza kwa makini.

Dakika 71,mshambuliaji Artem Dzyuba anaifungia Russia bao la tatu akiunganisha kwa kichwa krosi ya Aleksandar Golovin.

Mshambuliaji Denis Cheryshev alifunga bao la nne katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja katika dakika 90.

Jahazi la Saudi Arabia lilizidi kuzama baada ya Aleksandr Golovin kufunga bao la tano kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.