Ruzuku yatawala mkutano wa vyama vya siasa

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Mussa Juma Assad

Muktasari:

Hayo yamejiri katika mkutano ulioandaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo vimetaka vyama vyote vipatiwe ruzuku ya kujiendesha

Dar es Salaam. Vyama vya siasa vimesema itakuwa vigumu kwa baadhi yake kupokea hati safi ya mahesabu kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa sababu vingi havina fedha za ruzuku.

Wakichangia mada kwenye mafunzo ya namna ya kuandaa hesabu za vyama vyao kutoka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini leo, viongozi wa vyama hivyo walisema vyama vingi vipo taabani na havitaweza kutengeneza hesabu bila ya kuwa na fedha za kujiendesha.

Makamu Mwenyekiti wa Demokrasia Makini, Cecilia Augustino alisema vyama vingi vimekuwa vikihaha kujiendesha na wakati mwingine kuazima viti baa ili wakaguzi wakija waone kuna uhai.

"Hatuna fedha wala ruzuku, hatuna mali kule kwenye vyama, wakati mwingine hao wakaguzi wakija inabidi tuazime viti baa, hili suala liangaliwe," alisema.

Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee la Chadema, Roderick Lutembeka alisema lazima uandaliwe utaratibu wa kutoa kima cha chini cha ruzuku kwa kila chama kwa ajili ya kujiendesha.

"Haya tunayo fundishwa haitakuwa rahisi kuyatekeleza kwa sababu ukweli ni kwamba vyama havina fedha, unawezaje kukagua taarifa ya hesabu za vyama wakati haviingizi kitu? Lazima vyama vyote vipewe ruzuku," alisema.

Kaimu Katibu Mkuu wa ADC Dira ya Mabadiliko, Queen Sandiga alisema kama vyama vyote vitapewa uwezo wa kifedha vitaweza kujiendesha vizuri.

"Mnaweza kutufundisha masuala ya fedha ili baadaye mtuletee Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania) kuwa huko kuna rushwa, mafunzo haya ni muhimu lakini yaje kwa awamu na vyama vyetu vipate nguvu ya kifedha," alisema

Hata hivyo, Mhasibu Mkuu kutoka Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Christopher Mwisheswaswa alisema kuwe na ruzuku au kusiwe na ruzuku lazima taarifa  za hesabu ziandaliwe.

Alisema taarifa hizo ndizo zinazoonyesha uwazi wa vyama vya siasa kwenye mapato na matumizi.

"Mahesabu yanatengeneza uwazi kutoka kwenye vyama vyenu, mkitaka kuwa na vyama basi sheria hii lazima itekelezwe," alisema