SMZ kutumia Sh1.32 trilioni mwaka 2018/19

Wednesday June 20 2018

Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dk

Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dk Khalid Salum Mohammed akijibu maswali yalioulizwa katika Mkutano na waandishi wa Habari  kuelezea Mapitio ya Uchumi na Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali (2017/2018) na muelekeo wa uchumi na Bajeti kwa Mwaka 2018/2019. katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha Vuga mjini Zanzibar. Picha na Haji Mtumwaa 

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imepanga kukusanya na kutumia Sh1.32 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed alisema hayo jana alipokuwa anatoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mapitio ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 na mwelekeo wa uchumi na bajeti kwa mwaka ujao wa fedha ofisini kwake Vuga, Mjini Unguja.

Waziri huyo alisema makadirio hayo ni makubwa yakilinganishwa na Sh1.08 trilioni zilizoidhinishwa mwaka huu unaoisha.

Kati ya fedha hizo, alisema: “Sh807.5 bilioni zitatoka kwenye vyanzo vya ndani, Sh464.2 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo na Sh3.4 bilioni kutoka kwa wafadhili.”

Vilevile, alisema SMZ inatarajia kukopa Sh40 bilioni kutoka taasisi za ndani na nje.

Alisema Sh702.2 bilioni zitatumika kwenye matumizi ya kawaida na Sh612.9 bilioni zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Akieleza muelekeo wa uchumi kwa mwaka 2018/19 alisema pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.7 ukichangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula baada ya ununuzi wa matrekta 20 mapya.

Dk Khalid alitaja vipaumbele katika bajeti hiyo kuwa ni kuimarisha miundombinu ya barabara na nishati, kuendeleza sekta ya utalii, kuimarisha viwanda vidogo na ubora wa vifungashio.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, kujenga miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege na makaazi pamoja na miradi binafsi ya uwekezaji katika maeneo ya Nyamanzi, Fumba, Mtoni na Matemwe.

Alisema mwaka ujao wa fedha, Serikali itaimarisha sekta ya uvuvi na mifugo, huduma za kijamii zikiwamo elimu, michezo na majisafi na salama. Maeneo mengine alisema ni utawala bora, ajira na kuendeleza utafiti.

Kuhusu fursa za kiuchumi, Dk Khalid alibainisha maeneo maalumu ya maendeleo ya viwanda (Industrial Parks), kuendeleza wazalishaji wadogo na usarifi wa mazao ya kilimo.

Licha ya kuongeza ajira, alisema Serikali itaimarisha: “Utafutaji wa mafuta na gesi kwa kujitayarisha kupokea matokea ya uchumi wa sekta hiyo.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Khamis Mussa alisema ni vyema kwa watendaji na wananchi kwa ujumla kuwa na ari ya maendeleo katika utekelezaji wa bajeti hiyo ili kuyafikia malengo ya ukuaji wa uchumi uliotarajiwa pamoja na ustawi wa jamii.

Advertisement