Saa 10 katika kijiji cha ‘kichawi’ Gambosi

Mganga wa tiba za asili na kiongozi wa kimila wa kijiji cha Gambosi, Malosha Kufungile akizungumza na waandishi wetu. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

> Vifaa vya waandishi vyatambikiwa kabla ya mahojiano

> Wenyeji wakana uchawi, ila waonya anayefika kwa hila huona cha moto

> Ndani ya mitandao ya jamii, kiJiji cha Gambosi kimekuwa kikitajwa kama ‘jiji’ lenye mkusanyiko wa watu wanaoamini katika ushirikina na kuendesha mambo ya kichawi. Hata hivyo, unapofika kijijini hapo hadithi ni tofauti, licha ya kwamba kuna mambo mbalimbali ya kushangaza na kusisimua.

Bariadi. Kwa wakazi wengi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, jina la Kijiji cha Gambosi haliwezi kutamkwa bila ya kuongezea sifa za uchawi na maisha ya imani za kishirikina.

Ingawa wengi wamezoea kutamka Gamboshi wenyeji wanasema jina sahihi ni Gambosi na ndivyo ilivyoandikwa hata kwenye vibao vinavyoelekeza zilipo ofisi za Serikali ya kijiji na shule ya msingi kijijini hapo.

Gambosi iko takriban kilomita 60 kutoka mji wa Bariadi mkoani Simiyu, maisha ya wakazi wa kijiji hiki yanakupa picha ya sehemu ilisiyofikika kirahisi na isiyo na huduma kama elimu na zile za kiserikali.

Na ndiyo maana inaonekana kama ni kijiji cha kufikirika kutokana na simulizi za kishirikina na maisha ya hofu kwa wasio wenyeji.

Hayo yote yalifanya mimi na wenzangu tufunge safari ya kwenda Gambosi kushuhudia maajabu hayo.

Wakati tukiingia Gambosi, tukiwa na mlinzi maalumu wa safari za kuelekea kijiji hicho, tunaona jinsi kilivyo na uoto wa asili unaofanya mazingira mazuri ya rangi ya kijani.

Wakati tukiingia Gambosi, kunakuwa na hisia tofauti, baadhi wanasisimka mwili kufika kijiji ambacho kina simulizi za kukanganya na wengine wanaingiwa na hofu ya kukutana na miujiza waliyokuwa wakisikia.

Tukiwa bado tumegubikwa na mchanganyiko wa mawazo, ghafla dereva wa gari letu aina ya Suzuki Escudo anasimamisha kujizuia kugonga mti mkubwa ulio mbele unaoashiria mwisho wa barabara.

Mmoja wa askari watano tuliokuwa nao ni mwenyeji wa kijiji hiki ingawa si mzawa. Anaelezwa kuwa ni mwenyeji kutokana na kuongoza misafara mingi ya viongozi au wageni wanaokwenda Gambosi.

“Unajua si kila askari hufurahia safari za kuja Gambosi,” anasema askari huyo na kuongeza;

“Huku, wanatakiwa watu wenye mioyo na nia safi. Watu kama mimi wasiojihusisha na mambo ya ushirikina. Hiyo ndiyo maana kila safari huwa nateuliwa.”

Baadaye tunasikia sauti na baada ya kugeuka tunamuona kijana mrefu na mwembamba anayeonekana kama mwenye matatizo ya akili, jambo linalotufanya tuanze kuwa makini kushuhudia maajabu. Baadhi yetu wanapandisha vioo.

Ndani ya sekunde chache wanajitokeza watu wengine wawili. Mmoja mzee wa makamo anayefika na kusimama pembeni mwa gari bila kutusemesha na mwingine kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30.

Kijana huyu anafanya ishara ya kututaka tufungue vioo. Meneja Ngassa aliyekuwa akiendesha gari letu ambaye anatoka jamii ya Wasukuma kama walivyo wenyeji wa Gambosi anapata ujasiri na kuteremsha kidogo kioo, ndipo kijana yule anapomwelekeza arudishe gari nyuma kidogo na kuonyesha njia inayochepuka.

Kijana huyo anayeonekana aliandaliwa maalumu kwa ajili ya kutupokea anatuelekeza hadi Shule ya Msingi Gambosi ambako ndiko ugeni wetu ulipangiwa kufika.

Tambiko kabla ya mahojiano

Kazi ya kutambika inafanywa na ntemi (si mtemi kama wengi wanavyotamka), Malosha Kufungile, kiongozi wa kimila na mganga wa tiba za asili anayeheshimika kijijini hapo.

Sote tunatakiwa kuweka mezani vifaa vyetu vyote vya kazi kuanzia kamera, vinasa sauti, kalamu na notibuku (note book) ili vitambikiwe.

Kwa ustadi, Ntemi Kufungile anazunguka meza yenye vifaa vyetu vya kazi akiimba na kunyunyiza dawa ya majimaji kama ishara ya kuvitakasa na kuvibariki.

Hata sisi hatukusalimika. Pia, tulitambikiwa kwa kunyunyuziwa dawa mwilini na kwenye viganja vya mikono. Yote haya yanayafanywa hadharani na aliyetambulishwa kwa jina la Ntemi Kufungile, ambaye alisema yeye ndiye mwenyekiti wa waganga wa tiba asili Afrika Mashariki.

“Sasa mko salama. Mnaweza kuendelea na kazi zenu bila wasiwasi,” anatamka Ntemi Kufungile.

Uchawi na Gambosi

Swali kwamba uchawi upo katika kijiji hiki, ndilo lilikuwa la kwanza kwangu tunapozungumza na Ntemi Kufungile.

“Sisi si wachawi? Hayo ni maneno ya watu wasiofahamu historia yetu. Sisi ni watu tunaoheshimu, kulinda, kudumisha na kufuata mila na desturi,” anajibu kwa upole, huku wananchi waliotuzunguka wakitikisa kichwa kuashiria kukubaliana naye.

Hata hivyo, kiongozi huyo kijana mwenye umri wa miaka 34 mwenye wake watatu na watoto wanane, anasema wanatumia zaidi tiba ya miti shamba.

“Dawa zetu ni kwa ajili ya kujitibu. Ni dawa za kuokoa maisha ya watu,” anasema kabla ya kuongeza neno la kuchanganya.

“Pia, tunazo (dawa) za kutulinda dhidi ya adui.”

Anatamba kuwa yeyote anayefika Gambosi kwa hila na nia ovu, hukiona cha mtema kuni kwa ama kupotea njia na kurandaranda hadi kujikuta amerejea alipotoka au kupita kijiji hicho bila kuona nyumba wala wenyeji.

“Anayefika kwa heri kama mlivyokuja tunampokea kwa heri vilevile na wala hatapata shida yoyote. Ila ukija kwa nia ovu utakayokutana nayo utayasimulia,” anasema.

Lakini mtendaji wa Kata ya Gambosi, Mathew Shini anasema kwa mujibu wa hadithi za zamani, vitendo vya kishirikina vilikuwapo hasa kwa wanaoamini mambo hayo.

“Hivi sasa ushirikina umebaki historia. Kama upo ni sawa tu na maeneo mengine kama vile Sumbawanga na Tanga ambako pia kulisifika na hata sasa zinasifika kwa utamaduni wa miti shamba,” anasema Shini.

Itaendelea kesho